Huyu Benchikha anajiamini hatari

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amesema vijana wake wapo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Al Ahly na wanahitaji kupata mabao mengi nyumbani, ili kujitengenezea mazingira mazuri kufuzu nusu fainali.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Benchikha amesema amekiandaa vizuri kikosi chake kuelekea katika mchezo huo.

“Kuna tofauti kubwa nilipocheza dhidi ya Al Ahly nikiwa na US Alger na mchezo ule ulikuwa tofauti na huu. Ule ulikuwa mchezo mmoja tu, lakini sasa tunaenda kucheza michezo miwili, ambayo lazima tushinde ili kufuzu,” amesema Benchikha.

Amesema, Al Ahly ni timu kubwa lakini lengo lake ni kuhakikisha anaivusha Simba kwa mara ya kwanza kuelekea hatua ya nusu fainali.

“Lengo tulilojiwekea hapo mbele ni kufika nusu fainali na hatuwezi kufika bila kushinda mchezo wa robo fainali. Al Alhy ni timu kubwa, tunaiheshimu lakini lazima tutumie vizuri uwanja wetu wa nyumbani, ” amesema Benchikha.

Habari Zifananazo

Back to top button