Taasisi yaanzisha michezo kuhamasisha utunzaji mazingira

MBEYA; Shirika la Uhifadhi la Six Rivers Africa limezindua mashindano ya michezo kwa shule za msingi zilizopo Kata za Madibira na Miyombweni wilayani Mbarali yaitwayo Conservation Cup 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira ya hifadhi za Taifa na kupinga vitendo vya ujangili wa wanyamapori.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mariam Mnozya, amelipongeza shirika hilo kwa kuandaa mashindano hayo, akieleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.

Mnozya amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali iko tayari kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa na kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi na jamii inayowazunguka.
Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo kutoka Shirika la Six Rivers Africa, Justina Kizanye amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kutumia michezo kama jukwaa la kueneza elimu ya uhifadhi wa mazingira na kupinga ujangili.

“Lengo letu kuu ni kutumia michezo kuwaelimisha watoto na jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kupinga ujangili. Tunaamini kuwa tukiwajengea watoto uelewa wa masuala haya tangu wakiwa wadogo, watakuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi katika jamii zao,” amesema Kizanye.
Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha shule za msingi 14 kutoka Kata za Madibira na Miyombweni, ambazo ni Mkunywa, Ikoga Mpya, Nyamakuyu, Chalisuka, Kanamalenga, Iheha, Mahango, Nyakadete, Madibira, Mapogoro, Mapogoro B, Magigiwe, Msangaji Mpya na Mlungu.
Kupitia mashindano hayo, Six Rivers Africa inalenga kuunganisha michezo na elimu ya uhifadhi, ili kuwajengea wanafunzi uelewa wa mapema kuhusu wajibu wao katika kulinda mazingira, wanyamapori na rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



