ICC yaonya mateso makali Sudan

UHOLANZI:MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa tahadhari juu ya kuendelea kwa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu katika eneo la Darfur Magharibi, Sudan, ambako mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yameendelea kwa zaidi ya miaka miwili.
Naibu Mwendesha Mashtaka wa ICC, Nazhat Shameem Khan, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa hali ya kibinadamu imezidi kuwa mbaya, huku raia wakikumbwa na uhaba mkubwa wa maji na chakula, na miundombinu ya kiraia ikilengwa moja kwa moja na makundi yenye silaha.
“Viwango vya mateso kwa raia wa Darfur sasa vimefikia kiwango kisichokubalika,” alisema Khan na kuongeza kuwa njaa imeenea, hospitali zimeporwa, misafara ya misaada ya kibinadamu inashambuliwa na utekaji nyara, ubakaji pamoja na ukatili wa kijinsia umeongezeka kwa kasi.
Amesema kuwa ongezeko la makundi yenye silaha nchini Sudan limechangia kuvurugika kwa usalama wa raia, huku mashambulizi dhidi ya maeneo ya makazi yakiwa ni jambo la kawaida.
Mapigano nchini humo, yaliyolipuka mwezi Aprili mwaka 2023, yamesababisha vifo vya watu takribani 40,000 na wengine zaidi ya milioni 13 wakilazimika kuyakimbia makazi yao, wengi wao wakikimbilia nchi jirani kutafuta hifadhi.
Khan ameliomba Baraza la Usalama kuongeza juhudi za kidiplomasia na usaidizi wa kibinadamu ili kusaidia kuzuia maafa zaidi na kuhakikisha wahusika wa uhalifu wanawajibishwa kisheria. SOMA: WFP: Njaa yaua wakimbizi wa Sudan



