IJP Wambura apangua ma-RPC

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IJP), Camillus Wambura

MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania (IJP), Camillus Wambura amebadilisha makamanda wa polisi wa mikoa kwa kuwahamisha na wengine kupangiwa majukumu mengine.

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imeeleza kuwa katika mabadiliko hayo amemhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishibwamu kwenda makao makuu ya Polisi Dodoma.

Misime alieleza kuwa nafasi ya Tibishibwamu inachukuliwa na Salum Morcase ambaye alikuwa makao makuu ya Polisi Dodoma.

Advertisement

“Pia amemhamisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya Kamishna Msaidizi wa Polisi, Geofrey Sarakikya kwenda makao makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Michael Njera ambaye alikuwa makao makuu ya Polisi Dodoma.”

Misime alieleza kuwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah amehamishiwa makao makuu ya Polisi na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Makuri Imori.

“Aidha, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu amehamishiwa Kagera kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa huo na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Edith Swebe,” alieleza.

Misime alieleza kuwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampagale amehamishwa kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *