Ilani CCM yatekelezwa Z’bar, ajira zaidi ya 120,000 zazalishwa

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepiga hatua kwenye uwekezaji katika sekta mbalimbali ambapo miradi 424 iliyotekelezwa imezalisha ajira rasmi 22,382 na zisizo rasmi 100,000.

Aidha, uchumi wa Zanzibar umekuwa hadi kufikia asilimia 7.5 huku pato halisi la taifa likiongezeka na kufikia thamani ya Sh trilioni 6.3.

Haya yalibainishwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Hemed Suleiman Abdulla wakati wa kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Novemba, 2020 hadi Desemba, 2024.

Alisema serikali imetangaza visiwa 21 kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya uwekezaji na tayari visiwa 15 vimepata wawekezaji huku miradi 16 imewekezwa ya thamani ya Dola za Marekani milioni 377.5. “Visiwa vitatu vimeshaanza ujenzi na Kisiwa cha Bawe kimeshaanza shughuli zake.”

Alisema hadi sasa zaidi ya miradi 424 ya thamani ya Sh bilioni 5.9 tayari imeshasajiliwa na kuzalisha ajira rasmi zaidi ya 22,382 na ajira zisizo rasmi zaidi ya 100,000.

Alisema pia serikali imeanzisha ‘logistic parks’ kwa eneo lenye ukubwa wa hekta 4.5 katika eneo Huru la Uchumi la Uwanja wa Ndege wa AAKIA unaokusudia kujenga jumla ya maghala 20 kwa awamu tofauti ambayo kwa sasa yanaendelea na ujenzi huo.

Aidha, Abdalla alisema uwekezaji wa miradi ya hoteli za nyota tano umeongezeka ambapo kwa sasa kuna miradi 41 ambapo miradi 14 imeshakamilika na 27 inaendelea na ujenzi ya thamani ya Dola za Marekani 857,712,806.8. “Kukamilika kwa miradi hii kutaongeza pato la taifa na kuzalisha ajira zipatazo 2,560,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button