‘Ilani zibebe Dira 2050’

OFISI ya Rais, Mipango na Uwekezaji imeshauri vyama vya siasa nchini kuweka Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuwa sehemu ya ilani za vyama ili kuwa na mwelekeo mmoja na kufanikisha malengo ya dira hiyo.
Pia, viongozi wa vyama vya siasa nchini wameshauri kuwe na elimu ya kodi ili kuondoa sintofahamu kati ya walipa kodi na serikali na kuitaka dira hiyo kuainisha sheria kali juu ya masuala ya rushwa kwani yanarudisha nyuma taifa na ukosefu wa haki.
Hayo yalielezwa jana katika Mkutano wa Vyama vya Siasa kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Dar es Salaam kujadili juu ya mambo ya kuongezwa na kutiliwa mkazo katika dira ili kuwa na mrengo unaofanana kwa vyama vyote.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema Dira ya Maendeleo ni ya Taifa na si ya serikali na ndio sababu kubwa wameanza na viongozi wa vyama vya siasa katika uhakiki wa dira hiyo.
Profesa Kitila alisema wanasiasa hawatakiwi kutofautiana wala kupishana katika mikakati ya maendeleo ya taifa kwa sababu chama chochote kinaweza kupata nafasi katika utekelezaji wa maendeleo na asilimia kubwa ya mambo yaliyowekwa katika dira ni mawazo na maoni waliyoyatoa kwenye kikao walichokifanya Agosti 21, mwaka huu.
“Sisi wanasiasa tusipishane kwenye safari ya maendeleo, hata nchi za wenzetu hawapishani mahali wanapokwenda lakini wanapishana katika mikakati ya kuwafikisha wanapokwenda, sisi katika mfumo wa vyama vingi unakuta bado tunapishana, nashukuru kwamba hilo tuna uwezakano tukafika,” alisema Profesa Kitila.

Aliongeza kuwa dira hiyo imeundwa kwa miundo minne na msingi mkuu wa dira ni amani, usalama na utulivu na mkondo huo upo mikononi mwa wanasiasa kwa sababu wana nguvu kubwa katika kuleta amani au kuivunja.
Aidha, aliahidi kufanyia kazi maoni ya wanasiasa hao katika rasimu ya pili itakayotolewa mwakani kabla ya kukabidhiwa kwa serikali ili kupitishwa katika bunge. Desemba 18, mwaka huu atakuwa na mkutano na vijana ili kujadili dira hiyo kwa upande wao.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume ya Mipango, Asha-rose Migiro alisema kinga madhubuti ya dira ya maendeleo ni ya kisheria na tayari imeshapatiwa ufumbuzi na kusema kuwa kinga ya pili ni kuiweka dira hiyo katika ilani za vyama ili kuwa na mrengo unaofanana.
Aliwataka wawasilishe michango na mitazamo yao kwa njia ya maandishi ili waweze kufanya yaliyo sahihi wanapotoa rasimu ya pili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo kwani kufikia Januari 18, 2025 wanatakiwa kuwa wamekamilisha uhakiki wa rasimu hiyo ya kwanza.
“Dira hii iwekwe katika ilani za vyama na mlisema dira hii itafutiwe kinga ya kisheria, wengine mlisema suala la kuweka kikatiba, sasa kinga madhubuti inakuja lakini tungependa kinga ya pili ni kuangalia mambo haya makuu katika ilani zenu za vyama,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliunga mkono hoja hiyo na kusema kuwa ni jambo la msingi na kuahidi kulituma kwa waandaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025 kuzingatia mambo yaliyopo katika dira kwa sababu imezungumzia demokrasia na katiba iwekwe katika utekelezaji wa haraka.
“Nimelituma kwa watu ambao wanaandaa ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2025 kwamba kuna mambo ya msingi ya kuweza kuzingatia kuonesha kwamba chama kinachosimamia haki sawa kwa wote kitatekeleza mambo muhimu, kwa hiyo agizo lako kwamba sisi kama vyama tunatakiwa kushiriki katika kutoa michango katika dira hii basi tuweze kuitumia katika kutumia ilani zetu,” alisema Profesa Lipumba.
Pia, alisema uwepo mkakati kupambana na jambo la elimu kwenye uchangiaji wa kodi, kwani kunaonekana kuwa na sintofahamu japokuwa kuna mikakati inawekwa lakini fedha zinaonekana hazitoshi ingawa kodi zinakusanywa na kwa walipakodi nao wanalalamika kuwa kodi ni kubwa, hivyo kukiwa na elimu juu ya suala hilo itasaidia kuondoa mkanganyiko huo.
Mdau wa masuala ya siasa, John Cheyo alisema dira haijazungumza sana kuhusu suala la rushwa kwani rushwa imeharibu mambo mengi na kuchangia ukosefu wa haki na kusababisha kurudisha nyuma taifa katika maendeleo, hivyo ikizungumza kuhusu sheria kali itasaidia kupunguza suala la rushwa nchini kufikia 2050.



