INEC yaeleza sababu kuongeza muda Dar

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeongeza siku mbili kuboresha daftari la kudumu la wapigakura mkoani Dar es Salaam kuanzia leo.
INEC imetangaza kuwa baada ya siku hizo, haitaongeza muda zaidi.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele alitangaza uamuzi huo kutokana na mwitikio wa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam tangu kuanza uboreshaji huo Machi 17, na ulitarajiwa kumalizika jana.
“Kutokana na mwitikio mkubwa, tume ilichukua hatua za kuongeza mashine za BVR kits pamoja na watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi na hatua hii imewezesha zoezi kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote,” alisema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele amepongeza wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mara ya kwanza, kuboresha au kuhamisha taarifa zao na kupata kadi mpya kwa ambao kadi zao zimepotea au zimeharibika.
“Napenda kuwakumbusha kuwa zoezi hili halihusishi ubadilishaji wa kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 kwa kuwa kadi hizo ni halali na zitaendelea kutumika kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema.
Aliongeza: “Wananchi wote ambao kadi zao hazijaharibika au kupotea, hawajahama kutoka kata au halmashauri hawahusiki na zoezi hili.”



