Inec yazidi kunoa wanahabari Uchaguzi Mkuu

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema imejipanga kushirikiana na vyombo vya habari kuhakikisha habari na maudhui yake yanalenga kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema hayo jana mkoani Dar es Salaam alipomwakilisha Mwenyekiti wa Inec, Jaji Jacobs Mwambegele kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari.

Kailima alivitaka vyombo vya habari kuepuka habari za upotoshaji na badala yake visambaze habari za kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi badala ya kuleta machafuko.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, INEC itashirikiana kikamilifu na vyombo vya habari kuhakikisha maudhui yote yatakayopelekwa kwa wananchi yanalenga kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.

“Tume itaendelea kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu uchaguzi Kadiri inavyowezekana na itakutana na wanahabari mara kwa mara kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu uchaguzi,” aliongeza Kailima.

Aidha, alisema Inec itaendelea kushiriki katika vipindi mbalimbali vya televisheni na redio kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ili kuwarahisishia wananchi kushiriki kwenye uchaguzi.

Kadhalika, Kailima aliwakumbusha waandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na kuchuja maudhui yao ili kutowalisha wananchi maudhui ya kupotosha na kujenga chuki kati yao na wagombea.

Katika hatua nyingine Kailima alisema kuanzia Septemba 1, 2025 Inec itafungua dirisha la mfumo maalumu ambao utaruhusu chombo cha habari kutoa maombi kwa waandishi wake waruhusiwe kuingia katika chumba cha kupigia kura.

Alisema ili kutoa nafasi kwa wananchi kupata habari zaidi za uhakika, Inec inakamilisha kujenga studio zake za televisheni na redio mkoani Dodoma zitakazotumika kutolea taarifa za tume.

Alieleza ratiba ya utoaji wa fomu za wagombea wa kiti cha urais kuwa zitaanza kutolewa Agosti 9 hadi 27, mwaka huu na zoezi litafanyika makao makuu ya tume mkoani Dodoma.

Alisema kuanzia Agosti 14 hadi Agosti 26 mwaka huu itakuwa ni zamu ya wabunge na madiwani kuchukua fomu na kurudisha katika ngazi ya jimbo na kata na Agosti 27, itakuwa ni uteuzi wa wabunge na madiwani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button