Iran yatoa masharti mapya ya Nyuklia

TEHRAN, IRAN : WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema Marekani inapaswa kulipa fidia kwa hasara iliyosababishwa na mashambulizi wakati wa vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel, kabla ya kurejea kwenye mazungumzo ya nyuklia.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Financial Times yaliyofanyika mjini Tehran na kuchapishwa Alhamisi, Araqchi alisema Iran haitarejea katika hali ya kawaida bila majibu ya wazi kutoka kwa Marekani kuhusu uhusika wake katika vita hivyo. “Marekani lazima ieleze kwa nini ilitushambulia katikati ya mazungumzo, na ihakikishe kuwa hilo halitatokea tena. Pia, ni lazima ilipe fidia kwa uharibifu uliotokea,” alisema.
Araqchi, ambaye ni mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia, alibainisha kuwa kulikuwa na mawasiliano kati yake na mjumbe wa Marekani, Steve Whittaker, wakati na baada ya vita hivyo. SOMA: Iran yasitisha ushirikiano IAEA
Amesema ujumbe wa Iran ulisisitiza kuwa suluhisho la ‘ushindi kwa pande zote’ ndilo litakaloweza kuondoa mkwamo wa muda mrefu wa mazungumzo ya nyuklia. “Machaguo ni machache, lakini yanawezekana. Tunahitaji kuhakikisha kuwa upande wa pili una nia ya kweli kufikia makubaliano ya haki kwa wote,” alieleza Araqchi.



