Iringa yaongeza kasi usajili Bima ya Afya kwa Wote

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewaonya viongozi wa halmashauri na wataalamu wa afya kutofanya zoezi la usajili wa Bima ya Afya kwa Wote kuwa la siku moja tu, akisisitiza kuwa usajili usiishie katika viwanja vya Mwembetogwa.

Akizindua awamu ya pili ya mpango huo katika viwanja hivyo vya Mwembetogwa mjini Iringa, James amesema uzinduzi ni mwanzo tu, na kazi kubwa iko mtaani.

“Baada ya uzinduzi huu kazi haijaisha. Hakikisheni wananchi wanasajiliwa kwenye mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili uwapunguzie mzigo wa matibabu. Hatutafumbia macho uzembe katika utekelezaji,” amesema James.

Katika awamu hii, Mkoa wa Iringa unalenga kuandikisha kaya 13,086 zenye jumla ya wanufaika 31,170 wengi wakiwa ni wale wanaotoka sekta isiyo rasmi kama wakulima, wafanyabiashara ndogondogo, mama na baba lishe – ambao wamekuwa wakilazimika kulipia matibabu kwa fedha taslimu.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Iringa, Agnes Chaki, amesema idadi hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhakikisha hakuna familia inayoanguka kiuchumi kwa sababu ya gharama za matibabu.

“Hivi sasa familia nyingi zinalazimika kutumia akiba, kukopa au kuuza mali ili kumtibu mgonjwa. Bima hii inalenga kupunguza changamoto hiyo,” amesema Chaki.

Hata hivyo, James amekiri kuwa upanuzi wa wigo wa bima lazima uendane na ubora wa huduma.

Oktoba 21, 2026, alifanya ziara ya kushtukiza katika vituo vya afya na kuhitimisha katika Hospitali ya Frelimo, ambapo alikuta hali kwa ujumla ikiwa shwari, lakini akatoa maagizo ya kuimarisha upatikanaji wa dawa na mapokezi ya wagonjwa.

“Ongezeko la wanachama lazima liendane na uwezo wa kuwahudumia. Dawa zipatikane, vifaa viwepo na mgonjwa ahudumiwe kwa heshima,” amesisitiza.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Credianus Mgimba, amesema mkoa umejipanga kupitia wakuu wa vitongoji na viongozi wa dini ili kufikia kila kaya.

Mpango huo ni utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 na unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoweka afya kama msingi wa uchumi imara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button