‘Itakuwa mara ya kwanza Tanzania Rais kupokea viongozi wakuu 25’

DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuvunja na kuandika rekodi ya kuwa Rais aliyepokea idadi kubwa ya Wakuu wa Nchi 25 kuhudhuria nchini kwa pamoja tokea Tanzania izaliwe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Wakuu wa Nchi 25, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na Naibu Mawaziri Wakuu 10 wamethibitisha kuhudhuria kwenye Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika utakaofanyika Januari 27 na 28 mwaka huu kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Tulipokea Wakuu wa Nchi 19 wakati wa Kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere mwaka 1999 na Wakuu wa Nchi 15. Wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019, mkiangalia idadi ya Wakuu wa Nchi katika mkutano huu ni kubwa ukilinganisha na matukio hayo mawili yaliyopita,” Balozi Kombo amesema.

Akizitaja nchi ambazo Wakuu wa Nchi zao wamethibitisha kushiriki kuwa ni Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guine Bisau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Nigeria, Djibouti na Gabon.
Makamu wa Rais watakaoshiriki ni kutoka Gambia na Benin. Mawaziri Wakuu kutoka Cote d’Ivoire, Uganda, São Tomé and Príncipe na Equatorial Guinea na Naibu Mawaziri Wakuu ni kutoka Eswatine na Namibia.
SOMA: Ajenda ya nishati safi inavyoibeba Tanzania
Waziri Kombo amesema mkutano huo ni mwendelezo wa matunda ya diplomasia ya Tanzania ambapo Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kutangazika barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Amesema mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki katika Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) uliofanyika Brazil Novemba 2024 na Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) na kupewa na nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya Bara la Afrika ni kielelezo cha diplomasia ya Tanzania kuimarika duniani.