Ajenda ya nishati safi inavyoibeba Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika uliofanyika Paris nchini Ufaransa, Mei 14, 2024 ukikutanisha viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

JANUARI 27, mwaka huu macho ya mataifa yote ya Afrika yataelekea Tanzania wakati Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati utakapoanza ukiwa umebeba ajenda kuu ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wote.

Mkutano huo uliopewa jina la Mission 300 (M300) unaongozwa na kaulimbiu inayosema: ‘Kuharakisha  upatikanaji wa Nishati Afrika’, ukiwa na malengo ya kujadili dhana nzima ya upatikanaji wa umeme kwa wote hususan katika nyakati ambazo viongozi wa Afrika wanasisitiza matumizi ya nishati safi na salama.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila maandalizi ya mkutano huo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 99.

Advertisement

Kuhusu idadi ya wageni na washiriki wa mkutano hio, Chalamila anasema ni takribani 1,400 na kwamba Tanzania
sasa iko tayari kupokea ugeni huo mkubwa wa viongozi kutoka mataifa 54 ya Afrika na viongozi wengine mbalimbali
wa kimataifa.

Tanzania itanufaika na mkutano huo hasa ikizingatiwa kuwa wakuu wa mataifa hayo wataidhinisha Mpango Mahususi wa Nishati wa Afrika, ambao wakuu hao wanakubaliana kufanya mageuzi yatakayosaidia kufikia lengo la upatikanaji wa nishati kwa wote kwa njia za kuaminika, nafuu na endelevu.

Takwimu za nishati kwa Afrika zinaonesha kuwa hadi mwaka 2022 asilimia 83 ya watu milioni 685 walikuwa
hawajafikiwa na nishati hiyo. Kwa msingi huo, mkutano huo unadhamiria kuhimiza kuchukuliwa kwa hatua mbalimbali, ikiwemo kuingia makubaliano ili umeme uwafikie watu milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

Katika mkutano huo wenye azma ya kuwafikia watu hao milioni 300, nchi 14 zitasaini Mpango Mahususi wa Nishati wa Afrika Awamu ya Kwanza.

Nchi hizo ni Tanzania, Malawi, Chad, Nigeria, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Niger,
Liberia, Msumbiji, Madagascar, Zambia, Mali, Ivory Coast na Mauritania.

SOMA: “Ifikapo 2034 asilimia 80 watumie nishati safi”

Katika mpango huo, Tanzania inatarajia kunufaika kwa kuongeza kiwango cha nishati ya umeme itokanayo na nishati jadidifu ikiwa ni pamoja na umemejua, upepo na jotoardhi, pia kuongeza ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya umeme kwa njia ya ubia yaani PPP, IPP na EPC.

Kufanyika kwa mkutano huo Tanzania ni matokeo ya juhudi za maendeleo na mageuzi yanayofanywa na serikali katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya nishati.

Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa kinara wa hamasa ya matumizi ya nishati safi ya
kupikia. Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika sera, mipango na mikakati ya serikali mbalimbali duniani.

Umuhimu wa ajenda hiyo unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira, athari za mabadiliko ya tabianchi
pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati chafu za kupikia.

Rais Samia ambaye ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, amejipambanua kuwa dhamira yake ni
kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Wakati Rais Samia akiweka mkazo huo, Lengo Namba 7 la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa linataka watu wote wapate nishati safi, nafuu, inayopatikana kwa urahisi, endelevu na ya kisasa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko akigawa mitungi ya gesi ya kupikia
kwa wajasiriamali wa Soko la Sterio Temeke mkoani Dar es Salaam kama sehemu ya
kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Hivi karibuni, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema pamoja na Afrika kuwa na ajenda ya nishati safi na kuweka mikakati ya kutumia nishati safi ya kupikia, bado kuna changamoto za upatikanaji wake.

Anasema bado matumizi ya kuni na mkaa ni changamoto kwa kuwa yamekuwa yakisababisha athari za kimazingira,  kiafya, kiuchumi na kijamii. Anasema katika hilo, Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikibuni na kutekeleza sera na mikakati yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na utunzaji wa mazingira.

Wakati akifungua Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia mwaka 2022, Rais Samia alielekeza kuandaliwa kwa mkakati wa taifa utakaotoa mwongozo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hilo lilitekelezwa kwa serikali kuandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaotoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Dk Biteko anasema mkakati huu unalenga kuhakikisha kuwa, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya
kupikia ifikapo mwaka 2034. Dk Biteko anasema utekelezaji wa mkakati huo umeanza kwa serikali kutoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 inayouzwa kwa nusu gharama ya awali ambayo inasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara.

Dk Biteko alibainisha hayo Septemba mwaka jana kwenye hafla ya kusainiwa mikataba ya ushirikiano wa utekelezaji wa Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yenye thamani ya Sh bilioni 50.98 kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza Tanzania (TPS) na wasambazaji wa gesi ya kupikia.

Pamoja na mambo mengine, hatua nyingine iliyofanywa na serikali ni kupiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100, zikiwemo magereza, shule na hospitali, badala yake zinapaswa kutumia nishati safi ikiwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe yaliyoboreshwa.

Tukirejea kwenye mkutano wa M300, inatarajiwa kuwa siku ya kwanza ya mkutano huo itashirikisha mawaziri wa sekta husika ambao wataidhinisha makubaliano na washirika wenza wa maendeleo ya sekta binafsi na kuangalia maeneo wanayoweza kuunga mkono malengo ya mkutano huo.

Siku ya pili mkutano utaanza kwa vikao vya wakuu wa nchi watakaoelezana maono yao katika ukuaji wa sekta ya nishati na ushirikiano wa kikanda na wataridhia Azimio la Dar es Salaam la Wakuu wa Nchi kuhusu Nishati.

Sambamba na hayo watasaini mipango mahususi ya kitaifa ya nishati kwa kipindi cha 2025-2030 ambayo nchi tajwa 14 zitahusika. Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Kamisheni ya Umoja wa Afrika.