“Ifikapo 2034 asilimia 80 watumie nishati safi”

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema matarajio ya serikali ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia.

Dk Bitoko amesema hayo katika Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia ambalo limeandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) na Benki ya Uwekezaji ya Tanzania (TIB) kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi zote za Serikali lililofanyika katika Hoteli ya Kwanza, Kizimkazi Zanzibar.

Amesema kuwa, suala la nishati safi ya kupikia imekuwa ni ajenda muhimu nchini na duniani kote na Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa ajenda hiyo Afrika kwa kuibeba kuanzia Novemba 2022.

SOMA: Serikali yasisitiza wadau kuwekeza nishati safi

Dk Biteko amesema lengo  la serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapika katika mazingira salama na kwamba hatua hii itawezekana kwa kupatikana kwa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu, inayopatikana na kutumika kwa urahisi.

“Nimefarijika sana kuona utekelezaji wa lengo hili kwa vitendo, nimeona teknolojia mbalimbali katika mabanda ya maonesho hapo nje na niendelee kuhamasisha ubunifu wa teknolojia zinazowezesha wananchi kupata nishati safi kwa gharama nafuu,” amesema Dk Biteko.

Vile vile, Dk Biteko amewapongeza wabunifu kutoka banda la ORXY ambao wamekuja na ubunifu kwenye mitungi ya gesi (LPG) kwa kuweka mita inayopima gesi ambayo inarahisisha gharama za kujaza gesi na kuwa nafuu zaidi.

SOMA: Serikali yawatoa hofu wadau nishati safi ya kupikia’

Pia, ametoa wito kwa viongozi wote wa serikali, siasa, dini na wa jadi waliopo katika maeneo mbalimbali kuunga mkono ajenda hiyo yenye nia njema ya kumkomboa kila Mtanzania na kwamba kwenye majukwaa yao, wasiliache nyuma suala hilo.

“Tuhakikishe watu tunaowaongoza wanaelewa vyema umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa kampuni zinazowajibika katika jamii zao kupitia Corporate Social Responsibilities (CSR) niwahimize kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mkakati kwa vitendo kwa kugawa vifaa vya nishati safi ya kupikia kwa wenye uhitaji. Naamini tukishirikiana wote kwa pamoja tutaweza,” amesema Dk Biteko.

Habari Zifananazo

Back to top button