WIZARA ya Nishati Imewatoa hofu wadau wa sekta binafsi kuwa serikali inathamini mchango wa matumizi yote ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo umeme, gesi, na nishati zingine zote, ambazo ni rafiki kwa mazingira na afya.
Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi wa maendeleo ya Umeme,Styden Rwebangila, wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba kwenye mjadala wa wadau wa sekta ya nishati waliokutana kujadili na kutathmini uelekeo wa sekta ya nishati ilipotoka, ilipo na inapoelekea baada ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 sambamba na changamoto zilizopo na namna ya kukabiliana nazo.
‘’Napenda kuwatoa hofu wadau wa sekta binafsi na Watanzania kuwa nishati safi ya kupikia inajumuisha nishati zote na sio gesi pekee kama wengine wanavyodhani,’’ amesema Kamishna Rwebangila.
Amesema Wizara ya Nishati inathamini mchango unaotolewa na wadau wa maendeleo hususani Umoja wa Ulaya kwa kufadhili miradi mbalimbali kwenye sekta ya nishati hususani nishati safi ya kupikia na itaendelea kushirikiana nao kwenye upangaji wa mipango mkakati na uendelezaji wa sera.
Pia Meneja mradi wa Nishati kutoka Umoja wa Ulaya, Massimiliano Pedretti, amesema umoja huo utaendelea kufadhili miradi ya nishati safi ya kupikia kupitia mfuko maalumu wa nishati safi kulingana na mkakati na utekelezaji kufikia azma ya asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034, kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Meneja mradi wa matumizi bora ya Umeme kutoka Shirika la UNDP, Aaron Cunningham amesema UNDP, iliamua kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania kwenye sekta ya nishati safi ya kupikia kuhakikisha pia inaanzisha programu hiyo, ili kuwe na matumizi bora ya nishati ya umeme kwenye vifaa vitakavyotumiwa na wadau na kuongeza kuwa tayari wameshaainisha viwango vtakavyotumiwa kwenye bidhaa aina tano kama vipoza umeme, jokofu, televisheni, feni,na majiko ya umeme ili vitumie umeme kidogo.
Amesema mradi huu unatekelezwa kwa pamoja na Wizara ya Nishati tangu walipoanzisha mwaka 2022 na wamekuwa bega kwa bega na shirika la viwango Tanzania (TBS), ili viwango hivyo vitoe unafuu wa matumizi ya umeme kwenye vifaa hivyo.