JAB kupeleka Polisi orodha vyeti feki

DAR ES SALAAM; BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania (JAB) imesema inaandaa orodha ya vyeti feki vilivyowasilishwa na waandishi wa habari ili kuomba kusajiliwa na bodi hiyo.

JAB ilisema itawasilisha vyeti hivyo Jeshi la Polisi ili wahusika wachukuliwe hatua.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Patrick Kipangula alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa mada kuhusu Maadili na Sheria kwa Waandishi wa Habari kwenye mafunzo ya waandishi wa habari na watangazaji kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na yalishirikisha pia maofisa polisi na wadau wengine.

Kipangula alisema hadi sasa zaidi ya waandishi wa habari 3,400 wamesajiliwa na bodi hiyo kwa maana ya kukidhi vigezo na kupata ithibati.

Alisema waandishi 400 wamewasilisha taarifa zao na zinaendelea kufanyiwa kazi ili kupata ithibati.

“Lakini pia wapo waliowasilisha vyeti feki sasa tunaandaa orodha yao na tutakabidhi kwa Jeshi la Polisi ili washughulike nao kwa sababu hiyo ni jinai na ina mamlaka ya kushughulikia,” alisema Kipangula.

Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017 ziliweka kiwango cha chini cha elimu kuwa ni diploma ya uandishi wa habari au mawasiliano ya umma.

Katika kifungu cha 50 (2) kimeweka katazo kwa mtu yeyote kufanya kazi ya uandishi wa habari kama hana ithibati na kusema kitendo hicho ni kosa la jinai na adhabu yake kwa atakayetiwa hatiani ni faini ya Sh milioni tano hadi Sh milioni 20.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi aliwataka wanahabari ambao bado hawajajisajili JAB wafanye hivyo kwa wenye sifa ili kupata ithibati ya kufanya kazi hizo.

Kipangula alisema waandishi wenye sifa na waliosajiliwa na JAB ndio watahusika kuripoti habari za uchaguzi huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button