Jafo: Kuzuia wageni biashara 15 si ubaguzi

SERIKALI imesema amri ya kuzuia wasio raia wa Tanzania kufanya biashara za aina 15 si ubaguzi na haiwazuii kuwekeza nchini.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo alisema hayo alipozungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) jana asubuhi.
Julai 28, mwaka huu serikali ilichapisha amri hiyo katika Gazeti la Serikali namba 487A iliyotolewa chini ya Kifungu cha 14A (2) cha Sheria ya Leseni za Biashara (Sura ya 101).
Kupitia amri hiyo, serikali ilizuia wageni kufanya biashara ya uuzaji wa bidhaa kwa jumla na rejareja, uhamisho wa fedha kwa simu, biashara za saluni isipokuwa za hotelini, ukarabati wa simu za mkononi na vifaa vya kielektroniki.
Biashara nyingine walizozuiwa wageni ni usafi wa nyumba, ofisi na mazingira na uchimbaji mdogo.
Nyingine ni shughuli za posta, usafirishaji wa mizigo ndani ya nchi, uongozaji watalii ndani ya nchi, uanzishaji na uendeshaji wa redio na televisheni, uendeshaji wa makumbusho au maduka ya vitu vya asili, udalali au uwakala katika biashara na mali isiyohamishika.
Dk Jafo alisema Tanzania haijazuia wawekezaji kutoka nje kufanya uwekezaji isipokuwa imeweka utaratibu kwenye baadhi ya biashara ndogo zifanywe na wazawa ili wageni wafanye uwekezaji mkubwa.
“Hili lina manufaa makubwa sana, kwanza kujenga uchumi pili halizuii wageni kufanya uwekezaji… hii si ubaguzi ni utaratibu… kusaidia wananchi wake huku ikitengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji,” alisema.
Aliongeza: “Ilikuwa mgeni anaenda mpaka shambani moja kwa moja, anavunja mnyororo wa thamani ambao serikali imeweka uwekezaji mkubwa kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara wa kati waliokuwa wanachukua mazao shambani wanayalete sokoni, halafu mgeni akija aje sokoni kununua”.
Dk Jafo alisema serikali imeweka misingi imara ya kuvutia wawekezaji katika sekta za viwanda, utalii, uchimbaji mkubwa wa madini na katika sekta ya uchumi wa buluu.
Alisema wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam walibainisha maeneo 50 ya kufanyiwa kazi na baada ya kuyapitia serikali ilikuja na maeneo 15 yaliyotangazwa na kuwa sheria.
“Tulipitia sheria ya fedha ikapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Leseni na Biashara Sura 101 kumpa mamlaka waziri mwenye dhamana kuainisha biashara zinazopaswa kufanywa na zipi hazipaswi kufanywa,” alisema Dk Jafo.
Alisema sheria hiyo inatoa mwongozo kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kigeni kwenye biashara wanazopaswa na wasizopaswa kufanya.
“Kama tusingetibu janga hili katika miaka kumi ijayo, pale Kariakoo tusingekuta Mtanzania na usimuone katika sekta nyingine hizi ndogondogo, tungetengeneza janga kubwa kwa vijana waliokata tamaa, hawaoni serikali inawasaidia,” alisema Dk Jafo.
Alitaja malengo ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika miaka mitano ijayo ni kuona vijana wa Kitanzania wanafanikiwa katika biashara, kujenga uchumi wenye ushindani na rafiki na kuhakikisha wanakuja wawekezaji katika miradi mikubwa.
Hivi karibuni, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda alisema serikali imezuia biashara 15 kufanywa na wageni ili kulinda biashara za ndani na viwanda vya Tanzania.
Mwenda alisema kumekuwa na malalamiko kutoka nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa bidhaa zao zimezuiwa kuuzwa nchini.
“Wenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaona tumezuia biashara zao kuingia hapa, lakini kweli tunalinda viwanda vyetu kwa sababu wanatulipa kodi na hatuwezi kuruhusu bidhaa za nje zinazofanana na zetu, zikauzwa kwa bei nafuu sana, kuingilia soko kwa gharama isiyo ya haki,” alisema Mwenda.