Uwanja wa Jamhuri Dodoma ‘Out’ Ligi Kuu

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeuondoa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma katika orodha ya viwanja vinavyotumika kwa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/2025.

Taarifa ya Bodi hiyo leo imesema uwanja huo umeondolewa baada ya kupoteza sifa zilizoanishwa kwenye kanuni na sheria za mpira wa miguu.

SOMA: ‘Wasiotimiza vigezo vya uwanja bora, wawekeni pembeni’

Imesema eneo la kuchezea la uwanja huo limeonekana kukosa ubora ambapo sehemu kubwa haina majani ya kutosha na yaliyopo ni dhaifu jambo linaloufanya uwanja huo kutokuwa salama kwa wachezaji.

Kufuatia uamuzi huo, klabu ya Dodoma Jiji imetakiwa kupendekeza jina la uwanja mwingine miongoni mwa viwanja vilivyopitishwa kutumika kwa michezo ya ligi, kwa ajili ya michezo yake ya nyumbani hadi pale uwanja huo utakapokuwa umefanyiwa maboresho ya kuondoa mapungufu yaliyoanishwa.

“Bodi ya ligi inazikumbusha klabu zote kuhakikisha zinaendelea kutunza miundombinu ya viwanja vyao katika kipindi chote cha msimu wa ligi kwani kushindwa kufanya hivyo kutashusha ubora wa viwanja vyao na kusababisha viondolewe kwenye orodha ya viwanja vinavyotumika kwa michezo ya ligi,”imesema taarifa hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button