Jela miaka 20 kwa kukutwa na nyama ya pundamilia

MKAZI wa Kigongoni Katika Mji wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha, Waziri Mkomwa (32] amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela au kulipa faini ya shilingi milioni 27.5 baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na nyama ya pundamilia yenye thamani ya dola 1,200 sawa na zaidi ya shilingi milioni 2.7 za Tanzania.

Mshitakiwa alitiwa hatia kwa kosa hilo na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Arusha, Aisha Ndossy baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Mkomwa alikamatwa na nyama ya pundamilia Januari 20 mwaka 2019 Kigongoni Mto wa Mbu na askari wa wanyama pori baada ya kumwinda mnyama huyo bila ya kibali na kuuza katika maeneo hayo wakati akijua wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Awali mshitakiwa Mkomwa alifikishwa katika mahakama hiyo Februari 15 mwaka 2019 mbele ya Hakimu Anamalia Mushi na alimhukumu Februari 27 mwaka 2020 kwa kifungo cha miaka 20 na faini ya shilingi milioni 20 lakini mshitakiwa alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu hiyo.

Mahakama Kuu katika hukumu yake Juni 11 mwaka jana mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Arusha, Abdalla Mkama aliyepewa mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo na mahakama hiyo ya juu aliamuru kesi hiyo isikilizwe upya na hakimu mwingine na Juni 28 mwaka huu ilianza kusikilizwa na hakimu Ndossy.

Baada ya usikilizwaji huo mshitakiwa alikutwa na hatia na kujikuta akikabiliwa na kifungo cha miaka 20 au kulipa mara 10 thamani ya nyama hiyo ya pundamilia ambayo ni zaidi ya Sh milioni 27.5.

Mkomwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana mke na watoto wanaomtegemea na amekaa muda mrefu gerezani hivyo akaomba mahakama imwonee huruma.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Helen Osujaki aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ovu dhidi ya nyara za serikali kwa kuwawinda bila kibali wakati wakijua wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x