Jembe ni Mama kuwainua wanawake wakulima

MWIGIZAJI Irene Uwoya amemtakia heri Rais Samia Suluhu Hassan katika siku yake ya kuzaliwa hapo kesho na kutangaza zawadi aliyokuja nayo ni kuazisha kampeni ya mradi unaoitwa Jembe ni Mama lengo kuisaidia Wizara ya Kilimo kwenye kusukuma gurudumu la kilimo bora na chenye maslahi kwa wanawake.

Ujio wa mradi huo ni baada ya Irene kufanya uchunguzi mwaka 2018, juu ya nini anaweza kufanya kama kazi yake
ya pili na iwe biashara ya kujiingizia kipato katika maisha yake na kuchagua kilimo cha mpunga na tangawizi ambacho kimempa mafanikio.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Irene amesema mradi huu utasimama kwenye kumfichua, kumuinua na kumuwezesha mkulima mwanamke anayefanya kilimo duni katika jamii yake.

“Sisi kama Jembe ni Mama tunampa thamani mwanamke na kumfanya anufaike moja kwa moja na kilimo bila kuharibu misingi ya kifamilia na kwa utaratibu wa kilimo cha kisasa kinavyotaka, hivyo basi tutaanza na kutembelea wakulima wote wanawake ndani ya mikoa yote ya Tanzania.

“Tutatembea kila Kijiji,Tarafa, kata na wilaya kujua shida wanazokutana nazo wanawake hawa wanaojishughulisha na kilimo, ni jinsi gani wanaweza kufanya kilimo na pembejeo za kisasa na Jinsi gani wanaweza kuelimika juu ya biashara yao ya kwenye kilimo na wakaiona faida kwa manufaa yao, familia zao na taifa letu kiujumla,”amesema.

Amesema watakachofanya ndani ya kila mwaka watahakikisha wanawafikia idadi ya wanawake wengi wa kitanzania ambao ni Mashujaa wa kweli kwenye kilimo chao duni ambapo watawavumbua na watawaazishia miradi wezeshi na ya kisasa
ya wao kufanya mabadiliko ya kimkakati ya kilimo chao kutoka kilimo duni mpaka kilimo cha kisasa chini ya
uangalizi na usimamizi wa wizara ya kilimo. Amesema baada ya kuzunguka mwaka mzima kupata wanawake 26 kwa
kila mkoa Tanzania Bara na visiwani huko Zanzibar, wanatamani kama watapata nguvu ya uwezeshi.

Wanatarajia Jembe ni Mama watafanya tamasha kubwa kwa mkoa watakaouchagua litaitwa ‘JEMBE NI MAMA FESTIVAL”, ambalo litaonyesha mafanikio na hamasa kubwa kwa wanawake wapambanaji na wakulima kupitia kilimo chao na kuonesha thamani yao kama wanawake wenye mchango kwenye sekta hii kilimo katika taifa.

Amesema tamasha hili pia litatengeneza mtandao wezeshi na wa faida kwa wakulima wanawake na wakulima wote wadogo wadogo kwa wadau tofauti tofauti kwenye sekta hii ya kilimo.

“Nadiriki kusema hili tamasha litakua ni sikukuu rasmi ya wakulima wanawake Tanzania nzima, tunatarajia ndani ya miaka mitano mbele, tutakuwa na kundi kubwa la wannawake, wanaofanya kilimo cha kisasa na wezeshi, watakao kuwa na maendeleo makubwa kupitia kilimo chao na kuweza kusaidia familia zao,”amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button