Jeshi la polisi latakiwa kuwa macho usiku

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC) limewahimiza Jeshi la Polisi Usalama barabarani na Mamlaka Latra kuwa macho hasa nyakati za usiku msimu huu wa sikukuu ili kuhakikisha usalama kwa abiria wawapo safarini.
Aidha, limehimiza madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani kuepusha madhara yatokanayo na ajali zinazoepukika.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Katibu Mtendaji wa Latra CCC Daud Daudi amesema Jeshi hilo na Latra wanatakiwa kuhakikisha wako kazini muda wote kusaidia kuepusha ajali za barabarani.
“Jeshi la Polisi Usalama barabarani wanatakiwa kuhakikisha muda ambao unajulikana kama wasimamia sheria hawapo hasa nyakati za usiku ili kuwepo na usalama wakati wote kwa abiria wawapo safarini,”amesema.
Pia, kuhakikisha vyombo vya usafiri vyenye hitilafu havitumiki kutoa huduma za usafiri kwa kuhakikisha ukaguzi unafanyika kwa weledi, kutilia mkazo ufuatiliaji wa usalama wa vyombo na ufuataji wa sheria za usalama barabani kwa madereva wawapo safarini.
Amesema jambo la muhimu kwa abiria ni kuhakikisha wanafahamu viwango sahihi vya nauli iliyoidhinishwa na Latra, kufahamu muda, ratiba na kituo cha kuanzia safari lakini pia, ili kukwepa usufumbu kukata tiketi kwa njia ya mtandao.
Daudi ameongeza kuwa abiria wana haki ya kuelimishwa kuhusu huduma mbalimbali wakiwa safarini kwa kuwa kuna wengine husafiri mara moja kwa miaka na wengine ni mara ya kwanza wanahitaji kujua kama wanatakiwa wafunge mikanda, kutunza mazingira ndani nan je ya chombo.
Pia, ametoa rai kwa watoa huduma wategemee ongezeko kubwa la abiria ambao wengi wao sio wale ambao wamekuwa wakiwahudumia kwa siku za nyuma wawapatie ushirikiano na kuwapa huduma kwa uadilifu kwa kuzingatia matakwa ya leseni zao.



