Jihadharini na Kimbunga IALY – TMA

Upepo mkali, mawimbi kutokea

DAR ES SALAAM: WATUMIAJI wa bahari na wananchi wa maeneo ya ukanda wa pwani wametakiwawa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia pia kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

TMA imeeleza hayo katika taarifa yake kwa umma juu ya taarifa iliyotolewa Mei 17, 2024 na mamlaka hiyo kuhusu kuwepo kwa kimbunga “IALY” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.

“Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kimeendelea kuimarika na bado kimeendelea kusalia katika Bahari ya Hindi kama ilivyotabiriwa awali, hadi ilipofika saa 3 asubuhi ya Jumapili, Mei 19, 2024 kilikuwa umbali wa takriban kilomita 680 mashariki mwa pwani ya nchi yetu,” imeeleza taarifa hiyo.

Soma pia: https://www.malunde.com/2024/05/mwenendo-wa-kimbunga-ialy-katika-bahari.html

Kutokana na umbali huo kutoka nchini, vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2 vinaweza kujitokeza katika Bahari ya Hindi hususani kati ya Mei 19, 2024 na Jumanne Mei 21, 2024.

Soma pia: https://habarileo.co.tz/taarifa-mpya-kimbunga-hidaya/

Vilevile, vipindi vya mvua vinaweza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani hususani kati ya Mei 21 na 22, 2024.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

Habari Zifananazo

Back to top button