Jina la Kinjekitile Ngwale na Vita ya Majimaji

KABLA ya ujio wa Wajerumani kulikuwa na vitangulizi vya ukoloni. Hivi ni pamoja na ujio wa wamisionari na wapelelezi waliokusanya na kupeleka taarifa kwao kuhusu utajiri mkubwa wa mali uliokuwapo Tanganyika.

Wajerumani walipoanzisha utawala wao Tanganyika mwaka 1888, walikuta jamii zikiishi katika mfumo wa maisha ziliozoea. Ujio wa Wajerumani ulilenga hasa kuchukua ama kujipatia ardhi kustawisha mazao ya
biashara.

Miongoni mwa mazao ya yaliyoanzishwa na Wajerumani ni kilimo cha mkonge na pamba. Taarifa mbalimbali za kihistoria zinasema walivutiwa na mazingira na vyanzo vizuri vya kiuchumi vilivyopatikana katika mikoa ya Kusini Mashariki mwa Tanganyika.

Kusudi lingine la ujio wa Wajerumani lilikuwa kutafuta malighafi na wafanyakazi kwa ajili ya viwanda vyao huko Ujerumani. Kabla ya utawala wa Kijerumani, jamii za Tanganyika nyingi zilikuwa na taratibu zao za kulima mazao ya chakula na kumiliki ardhi yao.

Historia inabainisha kuwa, baada ya Wajerumani kuanzisha utawala wao, ardhi ilikuwa mali ya Serikali ya Kijerumani na waliwalazimisha wananchi kulima mazao ya biashara na kuwalipisha kodi.

Ingawa Wajerumami walijenga makanisa, shule, vituo vya afya na njia za usafirishaji kama vile reli na barabara ili kujiweka karibu na wananchi, lengo lao kuu lilikuwa kuleta utawala wao wa kidhalimu na kujitwalia rasilimali kwa ajili ya viwanda nchini kwao.

Hata hivyo, jamii nchini zilipokea ujio wa Wajerumani kwa mitazamo tofauti. Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho
ya Majimaji Songea, Balthazar Nyamusya anasema katika mazungumzo na HabariLEO kuhusu Vita ya Majimaji kuwa, tangu mwanzo Wajerumani walikuwa wamejawa na shauku ya kunyonya rasilimali katika makoloni yake.

Nyamusya anasema Wajerumani walivutiwa na vyanzo vya kiuchumi vilivyopatikana katika Mikoa ya Kusini – Mashariki mwa Tanganyika. Kwa mujibu wa Nyamusyal, katika kipindi hicho bila kutarajiwa Vita ya Majimaji iliibuka eneo la vilima vya Matumbi Kaskazini – Magharibi mwa Kilwa Julai, 1905.

Anaeleza katika vita hiyo, wananchi walikuwa wanapinga vitendo viovu hasa kulazimishwa kulima mazao ya biashara, kulipishwa kodi na unyanyaswaji uliofanywa na mfumo wa utawala wa Wajerumani.

“Waanzilishi wa mwanzo wa mapambano hayo walikuwa ni machifu wakishirikiana na Mganga wa Jadi kutoka
jamii za Wangindo na Wamatumbi,” anasema Nyamusya na kuongeza kuwa, baadaye viguvugu hilo lilienea kama
moto kwa jamii mbalimbali.

Jamii hizo ni pamoja na Wamatumbi, Wamwera, Wangindo, Wangoni, Wapogoro, Wandendeule, Wabena, Wasangu na nyingine nyingi ambazo zilizoamua kujiunga katika vita. “Wote kwa pamoja walipigana dhidi ya ukandamizwaji na kutakiwa kuishi, kulima na kuabudu kutokana na matakwa ya utawala wa Kijerumani,” anasema.

Nyamusya anaeleza jina la Majimaji lilitokanana imani ya matumizi ya ‘dawa’ iliyochanganywa na maji yaani punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani.

Mhifadhi kiongozi huyo anasema mwanzilishi wa vita hiyo alikuwa kiongozi aliyeitwa, Siikwako Mbonde alikuwa ni kiongozi na jemedari wa vita katika eneo la Kipatimu katika Kijiji cha Nandete mkoani Lindi. Anasema kiini cha kuanza vita hivyo ni wananchi katika eneo hilo waliamua kwenda eneo lingine la Kibata baada ya kuong’oa pamba iliyolazimishwa kwa ajili ya Wajerumani.

Nyamusya anasema Wajerumani waliposikia taarifa za kung’olewa kwa pamba walianzisha vita dhidi ya wenyeji wa maeneo hayo. “Baada ya Wajerumani kuanzisha vita, Wamatumbi na Wangindo walishirikiana kupingana na Wajerumani na ushirikiano wao ulitokana na kuwepo wa imani ya kidini,” anaeleza.

Anasema baada ya kuanza vita hiyo, kulikuwa na mtu ambaye ni mwanafalsafa (Kinjeketile ) na mwanafilosofia
mmoja (Siikwako) na kwa umoja wao walitumia maji kuwaunganisha katika vita ili wawashinde Wajerumani.
Kwa mujibu wa Nyamusya, kabla ya Wajerumani kuingia katika jamii za Wangindo na Wamatumbi walikuwa wanatumia maji hata wanapotaka kwenda kulima mazao yao.

Kwamba, walikuwa wanafanya masuala ya mila na desturi (matambiko) ili wafanikiwe katika kilimo chao cha
mazao mbalimbali ya chakula. Anasema ujio wa wageni hao na uamuzi wa kuazisha vita, uliwafanya wenyeji wa
makabila hayo watumie mbinu mbalimbali vita ikiwamo imani ya dawa kuwashinda Wajerumani.

Nyamusya anasema kulikuwa na mtaalamu mmoja wa tiba za asili ( Kinjeketile Ngwale) ambaye Wazungu
walimwita ni mchawi, lakini wenyeji walijua zilikuwa mila za kitamaduni za makabila yao.

Kwa mujibu wa masimulizi, waganga wa tiba za asili walikuwa na imani ya kuwaunganisha watu wao wakitumia dawa yenye mchanganyiko wa mbegu za mtama, punje za mahindi na kwa wakati fulani, walitumia mafuta ya nyonyo.

Nyamusya anasema alikuwepo bibi anayeishi katika Kijiji cha Nandete aliyekuwa mtaalamu wa mila na desturi
akiitwa Bibi Nantabila Naupunda. Bibi huyo kwa kushirikiana na Siikwako Mbonde aliyekuwa jemedari wa vita,
aliwashirikisha wapinganaji wengine na kuwahimiza kutumia hiyo dawa na ikapelekwa eneo la Kitaba.

Anasema Julai 15, 1905 waliwaendea wapiganaji wa Kijerumani kwa siku 15 na Wajerumani hao wakakimbilia eneo la Kilwa Kivinje. Vita hiyo ya Majimaji ilidumu hadi mwaka 1907.

“Kwa hiyo kwa kutumia hiyo dawa waliamini ya kwamba Wajerumani walishindwa na kukimbia kutoka kwenye kambi yao iliyokuwa makao ya Wajerumani hapo Kibata,” anasema.

Anasema huyo aliyeshughulikia kwa kutumia dawa hiyo watu wengi wanamjua kwa jina la Kinjeketile Ngwale, na hata katika vitabu vingi vya historia vimeandikwa na vinaeleza anaitwa Kinjeketile Ngwale kutoka Kijiji cha Ngarambe.

Anabainisha kuwa hivi karibuni wakati wanaendelea na tafiti zao kuhusu historia za ya Vita vya Majimaji kwa
kushirikiana na wenzao wa Makumbusho za Ujerumani, walikutana na kitukuu cha Kinjeketile Ngwale.

“Tukabahatika kukutana na kitukuu cha Kinjeketile Ngwale ndiye aliyetueleza ya kwamba babu yake ambaye ni
babu kama watano, alikuwa wanaitwa Nassoro Mohamed Kindamba Ali Ngwale,” anasema Nyamusya.

Mhifadhi mkuu huyo anafahamisha kuwa Makumbusho ya Taifa kwa sasa ipo katika mkakati wa kuandaa onesho la
historia Tanzania na Ujerumani, hivyo wanapita katika maeneo ambako vitu vya asili na kimila vilichukuliwa kutoka
katika jamii hizo.

Nyamusya anasema kwa mujibu wa maelezo ya wakazi wa Kijiji cha Nandete, Kipatimu jina hilo la Kinjeketile
lilikuwa ni bwawa. Wakazi hao wanasema bwawa hilo lilikuwa linatumika kwa ajili ya kuchukua maji ambayo yanachanganywa na mchanganyiko wa dawa na kuitwa ‘majimaji’ na ndiyo chanzo cha kupatikana jina la
Majimaji.

“Kwa lugha ya Wangindo na Wamatumbi wenyewe wanaita ‘mashi’ na walikuwa wakiita ‘mashimashi’ wakisema ‘Mashi ya Ngondo ya Mashimashi’ yaani ‘Vita vya Maji Maji,” anasema Nyamusya. “Wakati wakipigana,”
anasema, “Waliamuliwa kuyaoga maji hayo au kuyaweka katika paji la uso na kusonga mbele wakiamini kwamba,
wakiona wenzao wamedondoka, hao wenzao watanyanyuka tu baadaye kwa sababu ilikuwa inawapa imani.”

Anasema licha ya Vita ya Majimaji kusambaa kutoka Kipatimu eneo la Nandete, ilianza kwenda maeneo mengine ya Lindi na kusambaa hadi maeneo ya Mahenge wilayani ya Ulanga katika Mkoa wa Morogoro. Nyamusya anasema vita
ilisambaa na kujikita zaidi Songea ikipiganiwa na Wangoni. Huko, ilidumu kwa muda mrefu kutokana na kuwepo
upinzani mkubwa.

“Upinzani huo uliwafanya Wajerumani kuongeza nguvu na kikosi kingine kupigana na Wangoni,” anasema.
Akifunga sherehe za kuadhimisha Miaka 119 ya Vita ya Majimaji eneo la Nandete katika Kata ya Kipatimu wilayani Kilwa, Lindi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi anamsifu Rais Samia Suluhu Hassan
kwa kuenzi mchango wa wapigania uhuru na kuhifadhi historia ya Vita ya Majimaji.

Dk Abbasi anasema, “Wazee wetu walioongoza vita ile chini ya Jemedari Mkuu Siikwako Mbonde na mwanafalsafa wake mkuu na mhamasishaji Nassoro Mohamed Kindamba Ali Ngwale (anayefahamika kwa jina la Kinjekitile Ngwale).”

Anasema wazee hao walipandikiza mbegu ya ari ya uhuru na uzalendo ambayo hivi sasa Rais Samia anaienzi kwa kuleta maendeleo katika jamii kupitia sekta ya utalii. “Serikali yake (Samia) imeyatangaza rasmi kupitia GN 163 na 166 maeneo ya Nandete yaliyohusika na vita hiyo kuwa urithi wa taifa na wa kimataifa,” anaeleza Abbasi.

Naye Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana akiwa ziarani mkoani Ruvuma katika Makumbusho ya Vita ya Majimaji yaliyopo Songea, anasema wizara itaendelea kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kihistoria nchini.

Dk Chana anasema juhudi hizo kuwawezesha Watanzania kunufaika na mazao hayo ya utalii wa historia na
malikale.

Habari Zifananazo

Back to top button