Jiwe la Litembo, mto uliogeuka damu na historia ya Wamatengo 

RUVUMA; Ni majira ya mchana wa saa saba, mimi na timu yangu tunapoingia katika Kijiji cha Litembo, Kata ya Litembo Tarafa ya Mbuji wilayani Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma.

Lengo la kufika katika kijiji hicho ni kutembelea na kujua historia ya Jiwe maarufu la Litembo linalobeba historia ya kabila la Wamatengo na ushiriki wao katika Vita ya Majimaji iliyopigwa katika eneo hilo mwaka 1902.

Hapo tunakutana na Chifu wa Tarafa ya Mbuji, Hadrian Hyera, anatutambulisha kwa katibu wake, Bruno Kinunda ambaye ndiye anatueleza historia iliyoandikwa katika Jiwe la Litembo tangu mwanzoni mwa miaka ya 1900.

Kinunda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Makumbusho, Historia, Mila na Desturi za Wamatengo, Wilaya ya Mbinga anasema Litembo ni ngome ya kabila hilo ambalo asili yake ni mkusanyiko wa koo 42 zilizotoka katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi.

Anasema wapo waliotoka Malawi, Msumbiji na Tanzania maeneo ya Upangu.

“Malengo ya koo hizi katika eneo hili yalikuwa kukimbia migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao, baina ya makabila yao.

“Wengine walikimbia mapigano ya nchi na nchi, wengine walivutiwa na umaarufu wa Litembo kutokana na uwepo wa mapango mengi ambayo wangeweza kupata hifadhi,” anasema Kinunda.

Anasema wengine walivutiwa na uwepo wa uwanda wa misitu minene ambayo iliwanufaisha kwa kupata chakula kama mizizi, matunda na wanyama hasa kwa kuzingatia kuwa eneo hilo lilikuwa na wanyama wengi.

Litembo pia inasifika kwa kuwa na bonde lenye mito mingi midogo na mikubwa ambayo ilitumika kwa maji ya kunywa na uvuvi hasa kwa ile mito mikubwa, hali iliyofanya Wamatengo wavutiwe zaidi kuweka makazi katika eneo hilo.

“Kama nilivyosema awali kwamba nyumba ya kwanza ya mababu wakati huo ilikuwa ni mapango na vichaka, kwa hiyo Jiwe hili la Litembo lenye mapango ndani yake lilikuwa ni nyumba ya kwanza ya mababu hao,” anasema Kinunda.

Anasema baada ya kuishi kwenye mapango hayo kwa muda baadaye, walijenga nyumba za miti na kukandika udongo kabla ya kuhamia kwenye mfumo wa nyumba za udongo mtupu.

“…Baadaye wakatengeneza nyumba za matofali mabichi na hatimaye wakahamia kwenye mfumo wa sasa wa nyumba za kisasa za matofali,” anasema.

Asili ya neno Litembo kwa Wamatengo

Kanunda anasema mwonekano wa jiwe hilo lenye umbo la kichwa cha tembo ndiyo asili ya eneo hilo kupewa jina la Litembo.

“Asili ya Litembo baada ya koo hizi kukusanyika wakaona miamba hii ya mawe imekaa kama umbile la mnyama tembo, wale wazee wa asili wakasema eneo hili liitwe Litembo kutokana na maumbile hayo,” anasema.

Anaongeza: “Wamatengo wakaangalia jinsi misitu ilivyotanda, kwa lugha ya Kimatengo misitu ilikuwa inaitwa Itengo, misitu iliyotanuka walikuwa wanaita matengo basi wakasema hawa waitwe wamatengo (wanaoishi kwenye misitu minene).”

Anasema kwa kuwa zilikutana koo hizi 42 zilizozungumza lugha tofauti, waliamua kuungana ili kuwa na umoja na kutengeneza muundo wa uongozi uliokuwa na kiongozi mkuu wa pango aliyesimamia koo zote, Mkuu wa ukoo aliyesimamia koo moja moja na Bambu Mkulungu nafasi ambayo kwa sasa ndiyo chifu ambaye ndiye alipewa jukumu la kuunganisha lugha katika koo hizo kuwa lugha moja ya kimatengo.

Kinunda anasema silaha kubwa ya mababu hao ilikuwa kuishi pamoja ili kila linapotokea jambo, inakuwa rahisi kukusanyika na kukabiliana nalo.

Mto uliogeuka damu

Kinunda anaelezea historia ya Wamatengo walipovamiwa na Wajerumani na kuingia kwenye mapigano wakati wa Vita ya Majimaji na namna Wajerumani walivyoua mamia ya Wamatengo.

“Hapa mahali tulipo, bonde hili linaitwa Bonde la Kijito cha Mapyipi, kijito hiki kutokana na Vita ya Wajerumani na Wamatengo iliyotokea Machi 4, 1902 na mauaji yaliyofanywa na hawa Wajerumani kuwaua Wamatengo, damu zilizomwagika, zilikuwa damu nyingi sana… ziliganada katika kijito hiki na kuchukua kipindi kirefu,” anasema.

Anasema kwa takribani karne nzima maji ya mto huo yalishindwa kutumika kwa matumizi ya kunywa ingawa awali mto huo ulikuwa tegemeo kwa maji ya matumizi ya nyumbani.

Akielezea mkasa huo unaoelezwa kuchukua maisha ya takribani Wamatengo 800, Kinunda anasema picha ya maangamizi ilikuwa ya kusikitisha hasa kwa kuzingatia kuwa kijito hicho kilikuwa chemchemi ya uhai kwa eneo hilo na vijiji vya jirani hivyo maji yake kugeuka kuwa damu ilikuwa janga kubwa kwa Wamatengo.

Haikuwa vita ya silaha pekee

Ukatili wa wakoloni haukuishia tu kwa kuwaua Wangoni kwa risasi, bali hata kuchoma maghala ya chakula, kuteketeza nyumba na kuacha jamii nzima ikikumbwa na njaa.

Kinunda anasema kiongozi wa Wajerumani aliyejulikana kama Korongo, ndiye aliyetoa amri ya shambulio hilo baada ya Chifu Kawania wa Wamatengo kukataa kushirikiana naye.

“Baada ya mashujaa wetu kukataa kutawaliwa, Korongo alileta askari na silaha.

“Lakini mababu zetu walijipanga. Walijificha kwenye pango, wengine walikaa nyuma ya jiwe. Vita ikaanza. Lakini walizidiwa na risasi,” anasema.

Mwenyekiti wa Mila, Kata ya Litembo, Salvius Komba anasimulia; “Lile pango lilitumika kuhifadhi miili. Linaweza kuchukua watu 400 kwa wakati mmoja. Lakini idadi ya waliokufa ilizidi uwezo wake.”

Chifu Hyera akiwa mbele ya jengo la zamani la mahakama ambalo anatamani Serikali ijenge Makumbusho ya Litembo.

Anasema: “Hata leo ukichimba ardhini eneo hili, utakuta masalia ya miili, mifupa, vichwa, hadi mabaki ya silaha za jadi.”

Kutokana na historia hiyo muhimu, kilio kikubwa cha Chifu Hyera na wazee wa mila wa Litembo ni kujengwa kwa makumbusho ya Litembo ili historia hiyo itunzwe kwa faida ya vizazi vijavyo.

Chifu Hyera anasema kama historia hiyo itaendelea kuachwa hivyo ilivyo sasa, utafika wakati itapotea kabisa na hakutakuwa na wa kuihadithia au kuirithisha kwa vizazi vingine.

“Naomba serikali kulingana na historia kubwa iliyobebwa na eneo hili, itusaidie kujenga makumbusho ya kisasa katika eneo hili ili tuweze kuitunza vema historia hiyo iwe endelevu,” anasema.

Chifu Hyera anasema kwa sasa wanalo jengo la zamani lililokuwa likitumika kama mahakama wakati wa ukoloni ambalo linaweza kuboreshwa na kutumika kama makumbusho ya Litembo.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Litembo, Thedei Mpungu anaiomba serikali kuona umuhimu wa kujenga Makumbusho ya Litembo kutokana na uzito wa historia iliyobebwa na eneo hilo.

“Kutokana na historia iliyoelezwa hapa na Katibu wa Chifu naomba serikali iboreshe na kuimarisha eneo hili liweze kuwa eneo la makumbusho na litakuwa linaendelezwa kwa ajili ya kutunza historia ya Wamatengo ambayo ilianzia hapa kwenye haya mapango ya Litembo… tunatamani kuona makumbusho hayo yanawekwa hapa Litembo na tunaomba serikali iweke mkazo katika jambo hili,” anasema Mpungu.

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button