JK: Msuya hakuwa binadamu wa kawaida

RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya hakuwa binadamu wa kawaida.

Kikwete alisema hayo kwenye ibada ya maziko ya Msuya kijijini kwake Usangi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro jana. Msuya alifariki dunia Mei 7, mwaka huu kwenye Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

“Ni mvumilivu na lazima iwe kitu cha kuiga kwake. alikuwa Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Sokoine (Edward) alipougua na kwenda kwa matibabu. Aliporudi Mwalimu (Julius Nyerere, Rais wa Kwanza) akamwambia ampishe na yeye (Msuya) akarudi kuwa waziri wa kawaida, Waziri wa Fedha. Hii ilikuwa inataka moyo, ni jambo la kujifunza… huyu mzee ni mtu wa aina yake,” alisema Kikwete.

Alisema, Msuya alikuwa baba yake na mwalimu wake na amemsaidia mambo mengi kwenye safari yake ya uongozi, ikiwamo kumuelekeza namna ya kwenda kuzungumza na wafadhili Paris, Ufaransa warudi kuifadhili Tanzania mwaka 1994 alipoteuliwa Waziri wa Fedha chini ya Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi.

“Huyu mzee mimi ni baba yangu na amenilea,” alisema Kikwete na kuongeza:

“Alikuwa mshauri wangu nilipokuwa Rais na ushauri wake wala sio lazima umwite, akiwa na jambo unapata ujumbe anataka kukuona akifika anakueleza… siku nyingine anawasifia ‘mmejenga shule za kata nimefurahi’ siku nyingine anawagonga. Lakini kubwa katika yote hajaitisha mkutano na waandishi wa habari kusema serikali inafanya mambo ya hovyo”.

“Kazini na maishani alikuwa mwalimu wangu na mshauri… amenisaidia sana na namshukuru sana, nilishamshukuru akiwa hai na narudia tena leo akiwa amelala”.

Alikumbuka jinsi, Msuya alivyomsaidia yeye na waziri wake kupata usafiri wa kurudi ofisini kwao kutoka Ikulu baada ya kukosa usafiri kutokana na kuvunjwa kwa baraza la mawaziri.

“Mwaka 1990 Rais Mwinyi alivunja Baraza la Mawaziri… tulipotoka nje hakukuwa na magari na kwa sababu pale ndio tushapigwa ‘tanchi’ unaogopa hata kuingia ofisi yoyote kupiga simu ikabidi tutembee kwa miguu kutoka Ikulu mpaka barabarani kutafuta magari ya kutupeleka ofisini kwetu.

“Nashukuru wakati ule mitandao ilikuwa bado vinginevyo ingekuwa picha nzuri sana… kwa vile Mzee Msuya ofisi yake ilikuwa karibu pale na Ikulu (Wizara ya Fedha), basi tukatembea mpaka ofisini kwake akatupa magari ya kuturudisha ofisini,” alieleza.

Alimsifu, Msuya kuwa alikuwa kiongozi makini mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza na kulifafanua jambo gumu na kulifanya lieleweke na kuwa rahisi hata kwa mtu ambaye siyo mtaalamu wa uchumi.

“Alijipambanua, alikuwa mtu aliyejaaliwa akili nzuri, hakuwa mtaalamu wa uchumi na fedha kwa kusomea, lakini aliyafahamu mambo ya uchumi na fedha vizuri sana na ndiyo maana amewahi kuteuliwa Waziri wa Fedha mara mbili wakati wa Nyerere na mara moja wakati wa Mwinyi,” alieleza Kikwete.

“Lakini aliyafahamu vizuri sana mambo ya uchumi na fedha kama mchumi mbobezi, penye nia pana njia hili ndiyo la kwanza la kujifunza kwamba ukijitahidi kujifunza utajua ndiyo funzo,” aliongeza Kikwete ambaye amesomea uchumi na aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika Awamu ya Pili chini ya Rais Mwinyi.

Alisema sifa hiyo ndiyo ilimuwezesha, Msuya kusimamia vizuri uchumi katika vipindi vigumu kiuchumi nchini.

“Alikuwa waziri katika vipindi vigumu; cha kwanza uhaba mkubwa wa bidhaa madukani, lakini pia kulikuwa na uhaba fedha za kigeni, sababu uchumi ulikuwa umedumaa kulikuwa na changamoto kubwa za upatikanaji wa kiuchumi na kijamii, elimu, afya, maji, barabara,” alisema Kikwete.

Alisema, Msuya kama Waziri wa Fedha alikuwa na juhudi kubwa za kuzuia mambo yasiharibike zaidi wakati wa mtikisiko wa uchumi.

“Hakika alifanya kazi kubwa iliyotukuka alifanyaje, alikuwa anajua yeye zaidi, kitabu chake kinaandikwa basi pengine kwenye hicho kitabu tutanufaika sana,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button