JKCI kuanzisha kituo cha kupima moyo wachezaji

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete imeingia mkataba wa uzinduzi wa programu ya Moyo wa Michezo (Sports Cardiology Program) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa lengo la kuwapima wachezaji afya ili kuepusha vifo vya ghafla vinavyotokana na magonjwa ya moyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kusaini mkataba huo Rais wa TFF, Wallace Karia amesema program hiyo itahusisha uchunguzi wa afya ya moyo kwa wachezaji wote wa ligi kuu na ligi daraja la kwanza na mafunzo maalum kwa madaktari wa timu na wataalamu wa afya kuhusu magonjwa ya moyo yanayohusiana na michezo.
“Hii ni ndoto ambayo sasa inakwenda kutimia na Tanzania tunajiandaa kwa mashindano makubwa – CHAN 2025 na AFCON 2027, ambayo ni nafasi ya kipekee kwa taifa letu kuonesha uwezo wake katika kandanda na pia kuwekeza katika afya ya wachezaji wetu na TFF inatambua kuwa mafanikio katika michezo hayawezi kupatikana bila kuwa na wachezaji wenye afya bora hasa afya ya moyo.
Karia amesema wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa ya vijana hasa mashuleni na katika timu za mitaani kupoteza maisha ghafla uwanjani kutokana na matatizo ya moyo ambayo hayajawahi kugunduliwa
mapema hiyo ni hali ambayo hatuwezi kuendelea kuifumbia macho.
Amesema zoezi hilo litambatana na kampeni ya Sports Heart Marathon ili kujenga jengo la moyo ambapo TFF itatoa ushirikiano kamili katika maandalizi na utekelezaji wake.
“CAF na FIFA pia wamekuwa wakisisitiza juu ya umuhimu wa uchunguzi wa moyo kabla ya wachezaji kushiriki mashindano yoyote hivyo hii ni sehemu ya sera za kimataifa za ulinzi wa maisha ya wachezaji,hatuwezi kubaki
nyuma na tunajiunga na vyama vyote vya mpira duniani katika utekelezaji wa sera hii na kuanzisha sera mpya kua kila mwanamichezo kabla ya kujiunga na michezo lazima achunguzwe afya ya moyo nakuendelea kuchunguzwa kwa vipindi tofauti hii ni kwa ngazi zote hadi mashuleni.
Amebainisha kuwa bila programhiyo wanapata changamoto za kutojua hali ya afya za wachezaji,kupoteza vipaji kwa vifo visivyotarajiwa,kupunguza morali ya jamii kuwekeza katika michezo na hata kuathiri sifa ya nchi kimataifa pale mchezaji anapopoteza maisha kwenye uwanja wa kimataifa.
“Hilo ndilo tunalolisimamia na tuko tayari kusaidia katika ujenzi, vifaa, wataalamu, pamoja na kuhamasisha klabu zetu zote kushiriki kikamilifu.
Kwa upande wake Mkurgenzi wa JKCI ,Dk Peter Kisenge amesema takwimu zinaonesha kuwa mchezaji mmoja kati ya 50,000 hupoteza kila mwaka kutokana na matatizo ya moyo na wengine hushindwa kufika hospitali na wakati mwingine vifo kutokea mbele ya mashabiki na kuacha jamii kuwa katika mshangao.
“Leo tunazindua rasmi tawi la kadiolojia ya michezo lengo kuu ni kulinda mioyo ya wachezaji wetu ni mradi wa kipekee na wakwanza nchini kutokana na vifo hivyo tunafundishwa kwamba kila mchezaji anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina wa moyo kabla ya kushiriki kwenye mashindano yoyote.
Amesema kuelekea mashinfano ya AFCON 2027 wanahitaji kuwa tayari kuhakikisha usalama na ustawi wa kila mchezaji anayekanyanga ardhi ya Tanzania .
Dk Kisenge ameeleza kuwa mradi huo utakuwa katika tawi la JKCI-Dar group ambayo ipo karibu na uwanja wa taifa na uwanja wa ndege na litakuwa na vifaa vya kisasa,mabwawa ya kuogelea ,kumbi za mazoezi ,maeneo ya malazi kwa wanamichezo na huduma za uchunguzi wa hali ya juu na kisasa na ufuatiliaji wa moyo.
“Katika kuunga mkono mikakati ya ujenzi wa jingo hili jipya tutafanya Sports Hearth Marathon hivyo tutahasisha kila mmoja kushiriki kwa kukimbia,kuchangia au kueneza ujumbe huu muhimu na mbio hizi zitaanzia Masaki mpaka Hospitali ya Dar Group ambapo jingo hili litajengwa ,tutawakaribisha wanamichezo wote ,viongozi mbalimbali na watu wote kushiriki.



