JKCI yafanikisha matibabu Afrika

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu kuanzishwa mwaka 2015 imeokoa maisha ya zaidi ya watu milioni moja na kuokoa kiasi cha Sh bilioni 172 zilizokuwa zinatumika kupeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi.

Akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 10 ya huduma za matibabu ya moyo, Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, amesema taasisi hiyo inaendelea kupanua huduma zake na hivi karibuni itajenga hospitali ya moyo ya watoto yenye vitanda 100 katika eneo la Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

Dk. Kisenge alisema JKCI sasa siyo tu hospitali ya Tanzania bali pia ya Afrika, kwani wagonjwa kutoka nchi za Afrika na nje yake, ikiwemo India, Uturuki, China, Ufaransa na Ujerumani, wanapatiwa matibabu hapa. Aidha, taasisi hiyo imefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua, teknolojia ambayo ni ya kisasa duniani. SOMA: JKCI kuanza upandikizaji wa moyo rasmi

JKCI pia imekuwa na tafiti mbalimbali za kitaalamu na kuajiri watumishi kutoka Hospitali ya Dar Group, huku ikitoa huduma za tiba mkoba kufikia mikoa 16 ya Tanzania. Dk. Kisenge alisema JKCI inalenga kuwa “India ya Afrika” katika matibabu ya moyo, huku ikishirikiana na nchi za Afrika kama Zambia, Burkina Faso, na Comoro katika utoaji wa huduma na mafunzo ya matibabu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button