Joti, Leonardo wang’ara tuzo za ucheshi

MCHEKESHAJI mkongwe, Lucas Mhavile ‘Joti’ ameng’ara baada ya kutwaa tuzo mbili huku mchekeshaji Leonard Datus ‘Leonardo’ akishinda tuzo ya mchekeshaji bora wa jumla kwa wanaume na wanawake katika usiku wa Tuzo za Ucheshi (TCA) zilizofanyika Dar es Salaam juzi.
Joti alitwaa tuzo ya mchekeshaji bora wa mwaka na mchekeshaji nguli chaguo la watu wa mwaka.
Katika tuzo ya pili, Joti alichuana na wachekeshaji wakongwe akiwemo Bambo, Asha Boko, Mau Fundi, Mkwere, Kingwendu, Senga, Muhogo Mchungu na Brother K.
Kwa upande wa wanawake, Asma Jamida aliibuka mshindi wa tuzo ya Mchekeshaji Bora wa Kike huku Nanga Boy akishinda tuzo ya Mchekeshaji Bora wa Kiume wa Mwaka.
Katika tuzo hizo za kwanza,mchekeshaji chipukizi Dogo Sele alifungua dimba kwa kushinda kipengele cha ‘Best Funny Kid’
Aidha, Coy Mzungu mwanzilishi wa jukwaa la vichekesho ‘Cheka Tu’, alitunukiwa tuzo maalumu kwa mchango wake mkubwa katika kuleta mapinduzi kwenye tasnia ya vichekesho nchini.
Tuzo hiyo ilitangazwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, kama ishara ya kuthamini juhudi zake katika kuwapa fursa wasanii wa vichekesho kupitia jukwaa lake la Cheka Tu.
Jol Master aliibuka Mchekeshaji Bora Maalumu wa Mwaka. Hata hivyo alishindwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na matatizo ya afya.
Katika kipengele hicho, alishindana na wachekeshaji wengine wakali akiwemo Kipotoshi, Deo Matius na Nalim Joseph.
Katika kipengele cha Shoo Bora ya Runinga, kipindi cha ‘Kitim Tim’ kilijizolea tuzo, kikizishinda shoo nyingine maarufu kama Futuhi, Original Comedy na Mbambalive.
Kwa upande wa wachekeshaji wa ucheshi wa kusimama, Neila Manga aliibuka mshindi kwa upande wa wanawake akiwashinda Mambise na Mama Mawigi.
Wakati huohuo, Mc Eliud alitwaa tuzo ya mchekeshaji wa jukwaani mwanaume akiwashinda Leornado, Kipotoshi na Deo Rashid.
Katika kipengele cha Mchekeshaji Bora wa Kidijiti, Mama Mawigi aliibuka mshindi kwa upande wa wanawake huku TX Dulla akishinda tuzo hiyo kwa upande wa wanaume, akiwashinda Steve, Ndaro na Nanga.
Tuzo ya ‘Best Comedy Duo of the Year’ ilikwenda kwa Ndaro na Steve Mweusi ambao walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda Nanga na Shafii, pamoja na Zuli Comedy.
Mchekeshaji Aza Boy ameshinda Sh milioni tano katika kipengele cha mchekeshaji chipukizi wa mwaka 2025.
Kwa upande wa uigizaji wa vichekesho, Safina wa Mizengwe alishinda tuzo ya mwigizaji bora wa vichekesho wa kike, akiweka rekodi katika tasnia hiyo.
Katika hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alipewa tuzo ya ‘Champion of Comedy’, kama ishara ya kutambua mchango wake katika kuunga mkono sekta ya vichekesho nchini.
TCA 2025 inatajwa kuwa imeonesha ukuaji wa tasnia ya vichekesho nchini, kwa kutambua na kuthamini juhudi za wachekeshaji katika kuburudisha na kuelimisha jamii kupitia sanaa ya uchekeshaji.
Katika hafla hiyo Rais Samia Suluhu Hassan, ameikabidhi familia ya aliyekuwa mwigizaji mashuhuri wa ucheshi, Amri Athuman, ‘Mzee Majuto’, tuzo ya heshima ikiwa imeambatana na hundi ya Sh milioni 30.
Tuzo hiyo ni ishara ya kutambua mchango wa Mzee Majuto katika tasnia ya vichekesho nchini, ambapo alihusika katika kuinua vipaji na kuburudisha Watanzania kwa miongo mingi kupitia filamu na michezo ya kuigiza.



