JULIUS KAMBARAGE NYERERE: Shina la amani na ukombozi

NCHI za Afrika hasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara zitamkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama ‘amani’ na kinara wa ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika kwa kuzisaidia na hata kuongoza mapambano ya kung’oa wakoloni waliozikalia kwa mabavu.

Kada mbobevu na Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Kivule, Ilala mkoani Dar es Salaam, Kelvin Ndosi anasema mchango wa Nyerere ni mkubwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na anakumbukwa na Afrika na dunia kwa ujumla.

“Kutokana na kujitoa kwake, Nyerere atakumbukwa kwa mambo makubwa aliyoyafanya na yanayoendelea kuishi kwenye mioyo ya Watanzania na Afrika kwa ujumla,” anasema. Nyerere aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, alizaliwa mwaka 1922 na kufariki dunia Oktoba 14, 1999 wakati akitibiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa Ndosi, anakumbukwa pia kwa mchango wake kudumisha uhuru na amani nchini Tanzania na katika nchi mbalimbali Afrika ndiyo inayoifanya Tanzana iendelee kujulikana kama, ‘Kisiwa cha Amani’ na kuwa kimbilio la nchi nyingi kuhusu suala la amani.

Nyerere alikuwa kinara katika kudumisha ushirikiano na mataifa mbalimbali, hivyo kudumisha uhusiano mwema kwa kuunga mkono juhudi za vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika kufikia kujikomboa.

Katika juhudi hizo, Nyerere anaunga mkono juhudi za vyama vya siasa vya kupigania uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika kikiwemo cha FRELIMO (Msumbiji), ZANU-PF (Zimbabwe), ANC (Afrika Kusini) MPLA (Angola) na SWAPO cha Namibia na hata katika mataifa kadhaa ya Ulaya, Asia, Amerika Kusini na Kaskazini.

“Nyerere pia alishirikiana na vyama vya nje kama Chama cha Kikomunisti cha China (CPC),” anasema Ndosi na kuongeza kuwa, Nyerere aliamini uhuru wa Tanzania hauwezi kuwa kamili hadi nchi zote za Afrika ziwe huru.

Katika moja ya hotuba zake kuhusu ukombozi wa Afrika, Nyerere anasema: “Tukiimarisha ushirikiano wetu, tukielewa kuwa vita vyao ni vita vyetu, tutaongeza nguvu zetu za kuleta ukombozi wa Afrika nzima. Uhuru wetu hauwezi kuwa kamili kama jirani zetu hawajapata uhuru.”

Kutokona na mchango huo, nchi zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na wakoloni hatua kwa hatua zimepata uhuru ikiwemo Zimbabwe, Msumbiji, Angola, Namibia na Zimbabwe.

Tanzania pia ilikuwa kituo cha wapigania uhuru katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Nachingwea, Mazimbu Morogoro, Kongwa na maeneo mengine. Maeneo hayo pia yalitumika kuwapatia hifadhi salama viongozi wa vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika.

Katika uongozi wake, Nyerere anasisitiza wajibu wa kila taifa kuimarisha ushirikiano na kuungana mkono nchi zinazopigania uhuru barani Afrika. Aliamini kwamba nchi zote za Afrika zipo katika jahazi moja, lenye safari moja akimaanisha kuwapo hali na mazingira yanayofanana ya nchi hizo.

Licha ya Nyerere kuunga mkono harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na kwingineko hadi kufikia nchi malimbali za Afrika kujipatia uhuru, alishiriki pia utatuzi wa migogoro barani humo. Akiwa Mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa Mbele katika Ukombozi Kusini mwa Afrika, Nyerere pia alikuwa msuluhishi wa migogoro ya Burundi na Rwanda.

Hali hiyo imesaidia Tanzania kuwa na uhusiano mwema na majirani bila kujali itikadi. Alikuwa mshawishi mkubwa aliyetoa wazo la kuunda taasisi mbalimbali kuunganisha nchi za Afrika, ikiwa ni hatua kuelekea kuunda Afrika moja.

Hiyo ilichangia taasisi kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Ecowas, Comesa, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na taasisi nyingine ziliundwa ili kufikia azma ya kuunganisha Afrika. Taasisi hizo bado zinafanya kazi hadi sasa.

Ndosi anasema nchi za Afrika hasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara zitaendelea kumkumbuka Mwalimu Nyerere kwani alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Afrika inakuwa huru na mataifa yote yanaungana kutetea haki zao. Watu wengi ndani na nje ya Afrika wanaamini bila juhudi za Nyerere, huenda hadi sasa baadhi ya nchi za Afrika zingekuwa mikononi mwa wakoloni.

Kutokana na mchango wa Tanzania kuzikomboa nchi za Kusini mwa Afrika, imekuwa kivutio kikubwa cha wageni
wengi kutoka nje, kuanzia wanasiasa wa kimataifa na wasomi kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Marekani, Ulaya
Magharibu na kwingineko.

Historia ya Afrika inabainisha kuwa, Nyerere alikuwa na marafiki wengi waliofurahishwa na uongozi wake, akiwemo aliyekuwa Rais wa Zambia, Dk Kenneth Kaunda aliyesaidiwa katika jitihada za kuikomboa Zambia.

Kwamba, uhusiano baina ya Nyerere na Kaunda ulifanikisha azma ya biashara ya Zambia iliyokuwa ikiuza shaba China, Ujerumani na kwingineko kwa kujenga Reli ya Tazara kutokana na ufadhili wa Serikali ya China kutoka Dar es Salaam hadi ukanda wa shaba nchini Zambia.

Reli hiyo ni mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na China nje ya mipaka yao lakini pia ndiyo reli bora zaidi kujengwa duniani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Katika uhai wake, Nyerere aliimarisha uhusiano baina ya Tanzania na China ambao kimsingi, umeleta manufaa makubwa kwa nchi hizo.

Uhusiano mzuri wa Nyerere ulishamiri pia baina ya viongozi mbalimbali duniani. Mfano ni Rais wa zamani wa Benki ya Dunia, Robert Mac Namara aliyeiita Tanzania, ‘kipenzi’ chake cha Afrika. Hata Gavana wa Marekani, Jerry Brown alipotembelea Tanzania, alikaa juu ya magoti ya Mwalimu Nyerere kwa kile alichosema,

“Aweze kujifunza maajabu ya bara la Afrika kutoka kwa bingwa wa masuala ya Afrika na Dunia”. Tanzania inandelea kuaminika na kuwa kinara wa masuala ya diplomasia na amani duniani kote na kuifanya kuwa na uhusiano ulioimarika katika nchi mbalimbali.

Kimsingi, mchango wa Nyerere ulizidi kusambaa zaidi baada ya Uhuru wa Tanganyika, Desemba 9, 1961 na wakati wote wa utawala wake alikuza uhusiano wa kimataifa ambao utakumbukwa vizazi kwa vizazi.

Kwa harakati hizo za Nyerere, watu mbalimbali wanasema Waafrika kwa ujumla wao hawana budi kuendelea
kumuenzi na kumkumbuka kutokana na mchango wake katika historia ya ukombozi Afrika.

Ndosi anasema, Nyerere alikuwa kinara na nabii ambaye maono na utabiri wake unatakiwa kuenziwa kutokana na misingi ya taifa aliyoiweka na kuhakikisha nchi inapata maendeleo. Nyerere ameacha alama kubwa ya kuwa mmoja wa viongozi bora Afrika wanaopaswa kukumbukwa na kuenziwa kwa yale waliyoyafanya katika uongozi wao.

Wadau wa siasa na mambo ya kihistoria wanasema, Nyerere alifanya mambo mengi katika uhai wake yakiwamo kudumisha amani, kuunganisha na kuunga mkono juhudi za ukombozi na atakumbukwa kama nguli wa siasa Afrika na duniani.

Ndosi anahimiza vyombo vya habari kuendelea kuandika habari za kumuenzi Mwalimu Nyerere ili kuwezesha vizazi vijavyo kuendelea kudumisha aliyosisitiza Nyerere kama amani, haki, usawa, uadilifu, uongozi bora, siasa safi na watu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Ndosi anasema anamwomba Mungu, Tanzania ipate kiongozi kama Nyerere atakayehimiza amani, ukombozi wa kila Mwafrika na kuunganisha wananchi. Lingine analokumbukwa Nyerere, ni kujali ushirikiano na kutumia lugha ya Kiswahili kuunganisha Watanzania walio katika makabila zaidi ya 120.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. I get paid over (90$ to 500$ / hour ) working from home with 2 kids at home. I never thought I would be able to do it but my best friend earns over $22000 a month doing this and she convinced me to try. it was all true and has totally changed my life… This is what I do, check it out by Visiting Following web….
    .
    HERE——————————————⊃⫸ http://Www.Cash43.Com

  2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button