Kabudi atoa maagizo 7 bodi ya ithibati wanahabari

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, ametoa maagizo saba kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na kusisitiza umuhimu wa kufuata maadili ya taaluma hiyo ikiwemo kuimarisha sekta ya habari.
Prof Kabudi ametaka waandishi wa habari wafanye kazi kwa usalama, bila vitisho, unyanyasaji, au vikwazo visivyo vya lazima, kwani usalama wao ni msingi wa kudumu kwa vyombo vya habari.
Prof Kabudi ametoa maagizo hayo leo Machi 3, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo, ambapo amesisitiza kuwa bodi inapaswa kuwa mlezi wa waandishi wa habari kwa kuwapa miongozo inayohusu taaluma yao, wakizingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia uandishi wa habari ili kudhibiti uandishi usio na maadili.
Pia, amehimiza bodi hiyo kuandaa na kusimamia mfumo wa usajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia sifa za kitaaluma. Mfumo huo unatakiwa kuwa shirikishi, ukizingatia maendeleo ya teknolojia na mabadiliko katika sekta ya habari.
Aidha, bodi imetakiwa kuhakikisha waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma yao kwa kutoa miongozo na mafunzo ya mara kwa mara, ili kuwajengea ujuzi wa kisasa na kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Katika juhudi za kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa waandishi wa habari, Prof Kabudi ameagiza bodi hiyo kuandaa programu mbalimbali kwa wananchi, ili kuongeza uelewa wa mchango wa taaluma hiyo katika jamii.
Pia, bodi imetakiwa kuhakikisha waandishi wa habari wanatumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili. Hii inajumuisha kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.
Kwa maagizo hayo, Waziri Kabudi anatarajia kuona bodi hiyo ikitekeleza majukumu yake kwa weledi, kuhakikisha waandishi wa habari wanapewa mazingira mazuri ya kufanikisha kazi zao, huku wakizingatia viwango vya juu vya taaluma na maadili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando, akishirikiana na viongozi wenzake wameahidi kuwa watashirikiana ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu hayo kwa manufaa ya sekta ya habari na kuleta manufaa chanya katika sekta hiyo.



