Kadogosa ataja mbinu utekelezaji miradi ya maendeleo

KENYA: Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amesema Tanzania imejipanga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), kwa kujifunza uzoefu wa Kenya katika kuvutia uwekezaji na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo.
Kadogosa ameyasema hayo jijini Nairobi, Kenya, wakati wa Kongamano la 16 la Bara la Afrika kuhusu Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, akisisitiza kuwa mfumo huo unaweza kuongeza uwezo wa nchi kugharamia na kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu.
Amesema Tanzania inaendelea kuandaa na kutekeleza mikakati ya kutumia mfumo wa PPP katika miradi mbalimbali, hivyo uzoefu wa Kenya utasaidia kubaini mifumo bora ya utekelezaji, kuvutia wawekezaji binafsi na kukabiliana na changamoto za uwekezaji.

Katika mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa kongamano hilo, Kadogosa amesema wamejadili fursa za uwekezaji katika miradi ya barabara ya Kibaha–Chalinze, Chalinze–Morogoro, Morogoro–Iringa na Igawa–Tunduma.
Amesema pia wamejadili namna Kenya ilivyoanzisha Mfuko wa Taifa wa Miundombinu (Kenya National Infrastructure Fund), wenye mtaji unaokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni tatu, kwa lengo la kusaidia kugharamia miradi ya miundombinu na kupunguza vihatarishi vinavyoweza kuwafanya wawekezaji binafsi kusita kuingia katika miradi ya PPP.
Amesisitiza kuwa uzoefu huo unaweza kusaidia Tanzania kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kutafuta vyanzo endelevu vya fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka Kenya, Uganda, Ufaransa, Tunisia, Ivory Coast na Senegal kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufadhili miradi ya maendeleo barani Afrika.
Hatua hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kisasa na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya kimkakati.



