Kafulila ataka PPP ya ufanisi Dira 2050

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP) ni muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kafulila alisema hayo alipozungumza katika kipindi cha Twende Pamoja kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten.

“Sekta ya umma na binafsi zina mchango kwenye Dira ya 2050 na tunafanya ubia kwa sababu kuu tatu, moja ni kuvuta mtaji wa sekta binafsi, pili kuleta teknolojia mpya kwa sababu sekta binafsi popote duniani zimefika mbali kiteknolojia na sababu ya tatu ni kuleta ufanisi kiuendeshaji,” alisema.

Kafulila alisema katika ukuaji wa uchumi duniani mchango wa sekta binafsi hauepukiki na Tanzania si kisiwa hivyo kwa kuwa nchi imefungua uchumi haina budi kuwa na ushirika na sekta binafsi kukuza uchumi na biashara.

“Si Serikali ya Tanzania tu inafanya ubia hata serikali za nje zinafanya ubia kwa sabau una mchango na zimesaidia kufika mbali kimaendeleo,” alisema.

Kafulila alisema ubia katika taasisi za umma umeonesha matokeo chanya kwenye uchumi lakini pia nchi inapokea mitaji ya sekta binafsi na kuiwezesha serikali itekeleze miradi zaidi ya ukomo wa bajeti yake.

Alisema zipo sekta ambazo ni za kipaumbele kwenye uchumi na wabia wanazichangamkia lakini pia ziko sekta
za kusaidia uchumi ambazo wawekezaji hawazichangamkii kwa kuwa wanaona hazina mvuto ila katika ukuaji wa
uchumi zina manufaa na ndio maeneo ambayo serikali inayawekeza.

“Kuna miradi inalipa kiuchumi ila si biashara na hivyo ni muhimu serikali kuitekeleza mfano, Shirika letu la Ndege la ATCL linatengeneza hasara kihasibu, ila linatengeneza faida kiuchumi kwa sababu linasapoti sekta nyingine za uchumi, mfano; utalii na kuna baadhi ya sekta nyingine zina sura ya namna hiyo na lazima zitekelezwe,” alisema Kafulila.

Alisema katika hilo miradi ya PPP haina budi kutekelezwa kwenye Dira ya 2050 kwa sababu kupitia ubia huo sekta binafsi inaweza kutekeleza maeneo yenye mvuto na serikali ikatekeleza maeneo yasiyovutio lakini ni muhimu katika ukuaji wa uchumi na hivyo lengo la dira hiyo kutimia.

Kafulila alisema katika Dira ya 2050 malengo ni kujenga uchumi wa thamani ya Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na kusema hilo litafikiwa iwapo kila mmoja ataweka vipaumbele na mipango yake kwa kuzingatia malengo ya dira hiyo.

“Hadi sasa ni nchi 19 tu zina uchumi wa Dola trilioni moja na zaidi, katika Afrika hakuna nchi ya iliyofikia ukubwa wa uchumi huo isipokuwa Afrika Kusini. Hii ina maana kila mwaka tujenge uchumi kwa asilimia 10 hivyo lazima tubadilishe uwezo wetu wa kufikiri hili ni kwa sekta zote binafsi na umma na kuangalia upya sera na sheria ili ziendane na dira,” alisema.

Aliongeza: “Sekta binafsi ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wetu. Hatuwezi kujenga uchumi kwa kutegemea kodi lazima tushirikishe sekta binafsi, serikali imefanya marekebisho ya sheria mbalimbali kuruhusu ubia”.

Kafulila alisema wastani wa pato la mtu kwa kila Mtanzania ni kuwa lifike Dola za Marekani 7,000 mwaka 2050 na wastani huo unaonekana ni kidogo kwa miaka ijayo kwa sababu idadi ya watu inakua kwa kasi.

“Wastani wa ukuaji wa watu duniani ni asilimia moja, Afrika ni asilimia mbili, Tanzania tunaongezeka kwa zaidi ya asilimia tatu, athari yake ni kuwa kwenye nchi masikini inayoendelea kujijenga sehemu kubwa inakuwa ni mzigo kwa serikali kwa ongezeko hilo haitakuwa na uwezo wa kutoa afya, elimu na huduma za jamii,” alisema.

Kafulila alisema jamii haina budi kuchukua hadhari na kuzaa watoto wanaoweza kuwalea na si kuitegemea
serikali. “Kwa sababu katika hali ya kawaida si rahisi serikali kutoa huduma bora kwa ongezeko hilo ili hali nchi bado inaendelea kujijenga kiuchumi,’’ alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button