Kairuki aahidi kusimamia ujenzi shule mpya

DAR ES SALAAM: MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibamba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Angellah Kairuki amesema endapo atapata ridhaa ya wananchi kuongoza, atasimamia ujenzi wa shule mpya katika mtaa wa Upendo ili kuondoa adha ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Kairuki ameyasema hayo Oktoba 4,2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa kampeni za ubunge zilizofanyika katika viwanja vya Stop Over, ambapo alieleza kuhusu mipango ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Mkinipa ridhaa nitafuatilia utekelezaji wa miradi sita ya barabara, ikiwemo Kimombo, Taabu, Suka, Ukombozi na Peponi–KKT Temboni. Nitajitahidi kushughulikia changamoto ya ukosefu wa shule ya msingi katika mtaa wa Upendo, ambako watoto wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu na wakati mwingine hupata ajali,” amesema Kairuki.
Aidha, ameahidi kufuatilia ujenzi wa shule mpya katika maeneo ya Kimarabaruti, King’ongo, Mavurunza na Salaga, pamoja na kuongeza madarasa na madawati katika shule zilizopo.
Kwa upande wa miundombinu ya vivuko, Kairuki amesema atahakikisha kivuko maarufu cha mbao kinachotumiwa na wananchi wa Sanaa kinajengwa upya, pamoja na vivuko vya Majuzi na Chunga.
Akizungumzia wafanyabiashara wadogo, amesema serikali itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara wa bodaboda, bajaji na wamachinga kufanya biashara katika mazingira salama, huku akiahidi kufuatilia upatikanaji wa vyoo katika maeneo ya biashara yasiyo rasmi ili kuepusha milipuko ya magonjwa.
Kairuki ameongeza kuwa endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Kibamba, ataendelea kusimamia miradi ya afya, elimu, maji, barabara na uwezeshaji wananchi kiuchumi, sambamba na kuhakikisha miradi ya maji ya Bangu, Pasaka na Ruvu Chini inakamilika kwa wakati.
Amesema mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni ushahidi wa kazi kubwa iliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kutekeleza ilani yake bila kuchoka, akiwataka wananchi wa Kibamba kuendelea kukiamini chama hicho kwa maendeleo endelevu.
Akieleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chini ya serikali ya CCM, Kairuki alisema wamefanikiwa kujenga jengo la ghorofa mbili katika Kituo cha Afya cha Kimara kwa gharama ya Sh milioni 427, pamoja na kununua vifaa vya hospitali vyenye thamani ya Sh milioni 100.
Aidha, katika Zahanati ya Saranga, serikali imewekeza Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, ambalo linatarajiwa kuanza kutumika mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa upande wa elimu ya awali na msingi, amesema serikali ya CCM imewekeza Sh milioni 35.8 kujenga madarasa mapya na kutoa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi. Aliongeza kuwa katika shule ya msingi Jitihada, Sh milioni 100 zilitumika kuondoa kero ya wanafunzi kukaa chini.
Akizungumzia elimu ya sekondari, Kairuki amesema zaidi ya Sh bilioni 1.3 zimetumika kujenga madarasa 50, matundu ya vyoo 35, pamoja na ujenzi wa shule za sekondari za Ukombozi, Kigongona na Kisaranda kwa gharama ya shilingi milioni 377.
Kuhusu barabara, amesema zaidi ya Sh bilioni 1.8 zimetumika kujenga barabara za Kimombo, Suka, Kibongo, Sadaka na Sura, zikiwa katika viwango mbalimbali vya ujenzi, pamoja na mifereji ya maji ya mvua na kubainisha kuwa ujenzi wa kilomita 1.23 za barabara ya Kibanda cha Mkaa na Temboni Polisi unaendelea.
Katika eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi, amesema halmashauri imetoa mikopo ya zaidi ya Sh milioni 250 kwa vikundi 27 kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani, huku kaya 2,507 zikihudumiwa kupitia mpango wa TASAF kwa gharama ya Sh bilioni 1.697.
Kwa upande wa maji, Kairuki amesema wamefanikiwa kujenga tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 6, na sasa Jimbo la Kibamba lina uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 132. Alitaja miradi minne ya maji inayotarajiwa kutekelezwa, ikiwemo miradi ya Salama, Ukombozi, Kimara na Kibongo, ili kuongeza upatikanaji wa maji katika mitaa yote.