Kairuki aipa halmashauri Dar siku 7

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki ametoa siku saba kwa  wataalamu wa Halmashauri  ya Jiji la Dar es salaam kufanya tathmini ili kuangalia unafuu kwenye ujenzi wa shule katika maeneo yenye ufinyu wa ardhi.

Kauli hiyo ya Waziri Kairuki imekuja baada ya Mkuu wa Shule ya Msingi Kifuru jijini humo kuomba ridhaa ya kununua eneo lililopo pembezoni mwa shule hiyo au kubomoa majengo yaliyopo kwa ajili ya kujenga ghorofa  ili kusaidia kupunguza msongamano kwa wanafunzi shuleni hapo.

Kutokana na ombi hilo, Waziri Kairuki amesema serikali itajenga shule mpya na kuitaka Halmashauri kuhakikisha eneo hilo linapatikana na kuagiza kufanyika  tathmini ili kuangalia unafuu utakaosaidia kufanya maamuzi sahihi katika ujenzi wa shule hasa maeneo yenye ufinyu wa ardhi.

Mkaangalie kipi kitatupa tija na ufanisi, kipi kitatupunguzia gharama, kipi kitatusaidia bila kufifisha taratibu na sera zetu za elimu na miongozo mbalimbali ya elimu nchini mimi ninachotaka shule nyingine ijengwe kwa ajili ya kupunguza msongamano  wa wanafunzi.”

Amewataka wataalam hao kuhakikisha wanafanya tathmini ya kina itakayoonyesha kama Serikali itabomoa madarasa chakavu na kujenga ghorofa gharama zitakuwaje au kulipa fidia ili kutanua eneo husika kwa ajili ya kufanya ulinganifu.

Katika hatua nyingine,  Kairuki amemuelekeza  Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo  kuhakikisha  anatumia mapato ya ndani kununua madawati 500, viti, meza za walimu 47, kujenga matundu ya vyoo 25 ya shule hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button