Kamanda Mutafungwa awafunda Waganga tiba asili
MWANZA: Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa amewataka waganga wa tiba asili kushirikiana na Jeshi la Polisi Kuzuia matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi, mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, wizi pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Akizungumza katika mkutano na Waganga wa tiba asili zaidi ya 500 Desemba 22, 2023 jijini Mwanza, Kamanda Mutafungwa amewataka wataalamu hao kwenda kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka ili kuhakikisha wanapunguza matukio ya mauaji na uhalifu.
“Tunatamani kuona uhalifu unaisha katika Mkoa wa Mwanza ili ifike hatua matukio ambayo yamekuwa yakileta hofu katika jamii yetu yanaisha mfano mauaji kutokana na imani potofu za kishirikina, migogoro ya ardhi, matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, kuwania mali, unyanganyi, wizi, pamoja na utapeli na ndio maana tumewaita leo “…Alisema
Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) ,Yesaya Sudi amewaasa waganga wa tiba asilia kuwafichua waganga bandia wa tiba asilia na wapiga ramli chonganishi katika jamii kwani wao ndio wamekuwa chanzo cha kuchafua sifa ya taaluma hiyo.
Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asilia Mkoa wa Mwanza, Shabani Ramadhani akizungumza kwa niaba ya kundi hilo ametoa wito kwa waganga wenzake kutoa taarifa ya waganga wasiofuata sheria.