Kamati yapendekeza mapitio ya tozo Rocky City Mall
MWANZA: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imependekeza mapitio mapya ya tozo, ada mbalimbali zinazotozwa kwa wapangaji katika Kituo cha Biashara cha Rock City Mall cha jijini Mwanza sambamba na kuboresha mifumo ya jengo hilo ili kuvutia biashara zaidi.
Mapendekezo ya kamati, yamewatolewa na Mwenyekiti wake, Fatma Toufiq mwishoni mwa juma walipozuru jengo la Rock City Mall lililo chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutathmini maendeleo na maboresho yaliyofanywa hivi karibuni.
“Tozo za sasa kwa wapangaji zinahitaji kuangaliwa upya, kwa kufanya marekebisho na kuboresha michakato ya kiutawala, tunaweza kuhakikisha kuwa Rocky City Mall inaendelea kufanikiwa na kuvutia biashara zaidi, amesema Taufiq”
Walipowasili, wajumbe wa kamati walitembezwa kwenye ziara ya kina ya jengo hilo, ambapo waliona maboresho mbalimbali ambayo yameongeza mvuto na utendaji kazi wa jengo hilo kwa kiasi kikubwa na kupelekea ongezeko la viwango vya upangaji hadi kufikia asilimia 88.
“Mabadiliko yaliyofanyika hapa yanastahili pongezi. Ni wazi kuwa uongozi umewekeza juhudi kubwa katika kufanya jengo hili kuwa eneo lenye mvuto na linalofaa kwa biashara,” amesema Toufiq.
Ziara hii ya kamati ya bunge inaonesha nia ya serikali ya kusaidia miradi ya kibiashara inayochangia maendeleo ya kiuchumi ya ndani.
Rocky City Mall, kwa idadi yake inayoongezeka ya wapangaji na maboresho ya kimkakati, ipo tayari kuwa nguzo ya biashara jijini Mwanza.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii umeonesha shukrani zao kwa ziara na mrejesho wa kamati na kuahidi kutilia maanani mapendekezo hayo kwa umakini na kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufanya Rocky City Mall kuwa biashara yenye mafanikio zaidi, kwa wafanyabiashara na wanunuzi wa Mwanza.