Kamati yashauri kuharakisha ujenzi mkongo wa taifa

DAR ES SALAAM: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Serikali kuharakisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa unaounganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hatua hiyo itarahisisha Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kupanua huduma zake, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwanufaisha wananchi kupitia huduma bora za mawasiliano.

Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Kituo cha Data Center Mikocheni, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati, Selemani Kakoso, amesema utekelezaji wa mradi huo utaongeza ufanisi wa TTCL kujiendesha kibiashara.

Aidha, kamati imeishauri serikali kutoa zaidi ya Sh bilioni 70 kwa ajili ya maboresho ya kituo hicho, kufuatia miundombinu yake kuanza kuchakaa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Kairuki, amesema serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya mawasiliano inaendelea kukua kwa kasi, akisisitiza kuwa maoni yote yaliyotolewa na kamati yatazingatiwa kabla ya kuwasilishwa kwa randama ya bajeti tarehe 27 ya mwezi huu. Amesema maboresho ya miundombinu ni kipaumbele kikuu cha wizara yake.

Waziri Kairuki pia ameeleza kuwa wizara imeunda kamati ya kiufundi itakayoshirikiana na wataalamu kutoka DRC ili kukamilisha taratibu za kufikisha huduma za mawasiliano kupitia mkongo huo.

Sambamba na hilo, amesisitiza maboresho ya mfumo wa malipo wa Jamii Pay kwa kutumia QR Code ya kidijitali ili kurahisisha shughuli za kibiashara kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Katika kuimarisha zaidi sekta hiyo, Waziri Kairuki amefafanua kuwa Serikali inapanga kujenga kituo kikubwa cha kisasa cha kuhifadhi data jijini Dodoma, ambapo upembuzi yakinifu umekamilika na mashauriano na Wizara ya Fedha yanaendelea.

Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha ujao ili kuongeza usalama na uhifadhi wa taarifa za serikali.

Aidha, amesema kiasi cha Sh bilioni 30 kinatarajiwa kutumika kwa maboresho ya muda mfupi ya vifaa vya Data Center, huku serikali tayari imetoa ridhaa kwa TTCL kupata Dola za Marekani milioni 3.8 kwa ajili ya kuimarisha mitambo, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za mawasiliano nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button