Kamati za Bunge Afrika na uendelevu huduma za afya
HIVI karibuni ulifanyika Mkutano wa Wenyeviti wa Kamati za Afya kwa Mabunge ya Afrika uliojadili na kutathmini idadi ya watu na maendeleo hususani katika huduma za afya.
Mkutano huo ulitoa fursa kwa Wabunge wa Kamati za Afya za Mabunge ya Afrika kujadili kwa kina uhusiano wa huduma za afya na ongezeko la idadi ya watu barani humo.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel anasema umefika wakati kwa nchi za Afrika kuanza kutafuta majawabu katika matumizi sahihi ya rasimali ilizonazo ili kuinua huduma za afya za kibingwa na bobezi kwa kutumia teknolojia mpya na za kisasa.
Dk Mollel anasema ana matumaini kuwa, tafiti za kina, matumizi sahihi ya rasilimali na kuweka sera bora ni mambo
yanayoweza kuivusha Afrika katika suala la afya, ikiwemo afya ya mama na mtoto.
Naye Mbunge wa Singida Magharibi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya
Ukimwi, Elibariki Kingu anasema mkutano huo utafungua mawazo mapya juu ya sekta hiyo Tanzania na Afrika kwa
ujumla.
Akifunga mkutano huo, Spika wa Bunge la Tanzania ambae pia, ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk Tulia Ackson anawataka wabunge kutumia mkutano huo kuendeleza umoja uliopo na kushirikiana kutatua changamoto za kiafya zinazozikumba nchi nyingi za Afrika.
Anasisitiza uwajibikaji kwa wabunge ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta hiyo na nyingine katika mataifa yao.
“Mabadiliko yataanza na sisi wenyewe kama wabunge na watu wenye mamlaka ya kupanga na kuzisimamia Serikali zetu ili yale mazuri tunayoyatarajia yatokee basi yaanze na sisi kuwajibika katika nafasi zetu,” anasema Dk Tulia.
Kingu anasema moja ya maazimio ya mkutano huo ni kuzishauri serikali za Afrika kutumia rasilimali zilizopo kuwekeza zaidi kwenye sekta ya afya. Aidha, anasisitiza kusimamia ipasavyo bajeti zinazoelekezwa katika sekta
hiyo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
Maazimio hayo yanakwenda sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo pamoja na mambo mengine, inaelekeza serikali kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto na kuzitoa bila malipo ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Aidha, inaelekeza kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vifaa saidizi na vitendanishi kulingana na mahitaji katika ngazi zote za utoaji wa huduma bora za afya nchini.
Ilani hiyo pia inasisitiza kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji/sekta binafsi kujenga viwanda vya kuzalisha dawa, vifaa, vifaa tiba, vifaa saidizi na vitendanishi kwa kutumia malighafi zinazopatikana ndani ya nchi ili kupunguza mzigo kwa serikali wa kuagiza vitu hivyo kutoka nje.
Aidha, ilani pia inaelekeza kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya ili vitoe huduma bora zaidi kwa
wananchi.
Aprili mwaka huu Kamati ya Kudumu ya Bunge iliwasilisha taarifa yake ya utendaji na bunge likaazimia mambo kadhaa, ikiwemo kuitaka serikali iongeze wodi maalumu katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya huduma za watoto wachanga.
Aidha, liliazimia serikali kuongeza vifaa tiba kwa huduma za watoto hao pamoja na kuongeza wataalamu ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Kadhalika, bunge liliazimia kuwa serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu njia sahihi za kudhibiti malaria na itenge fedha za ndani za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa afua muhimu za udhibiti wa ugonjwa huo, ikiwemo afua ya matumizi ya viuadudu na viua viluwiluwi ili kudhibiti maambuzi zaidi.
Aidha, liliazimia kwamba serikali itekeleze kikamilifu mpango wa uendelevu wa mwitikio wa virusi vya ukimwi
(VVU) na upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI) nchini ili kupata rasilimali endelevu za ndani katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi bila kutegemea msaada kutoka kwa wafadhili.
Hili linakwenda sambamba na kuongeza jitihada katika kutoa elimu kuhusu njia bora za kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU kwa kuyafikia makundi maalumu, wakiwemo vijana na itoe elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia huduma za tiba na matunzo kwa wanaogundulika kuwa na maambukizi.
Bunge liliazimia serikali ihakikishe taasisi na sekta zake zinatenga fedha za kutosha kutekeleza mkakati wa kudhibiti
maambukizi ya VVU na kwamba, zishirikiane kwa karibu na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania kuratibu shughuli za udhibiti wa maambukizi ya VVU.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (TDHSMIS) unabainisha kuwa, vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa asilimia 80, kutoka vifo 556 kwa kila vizazi 100,000 hadi 104 na vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 100,000.
Matokeo hayo yanamaanisha mwelekeo mzuri wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ifikapo Mwaka
2030 ya kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kufikia 70 kwa kila vizazi hai 1,000.
Kwa mwelekeo huo wa majadiliano na maazimio ya mkutano huo, wadau wanasema Afrika inaelekea kuwa bara lenye uhimilivu na uendelevu katika kutoa huduma bora za afya na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Mkutano huo uliokutanisha mataifa 26 na maazimio yaliyofikiwa unakuwa chachu ya kuendelea kupungua zaidi kwa vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga na ni matumaini kuwa sekta ya afya Tanzania na Afrika itaimarika zaidi.



