Kamishna aipongeza NEMC kwa uadilifu katika utumishi wa umma

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Dk Laurean Ndumbaro amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kuendelea kuonesha uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi ofisi za Baraza Dk Laurean Ndumbaro amesema uadilifu uliooneshwa na Baraza hilo ni mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine za Umma katika kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.

SOMA: Nemc yashiriki mkutano jukwaa utunzaji mazingira

Amesisitiza kuwa uadilifu ndio nguzo kuu ya utumishi wa umma na ndio msingi wa kuaminika kwa Serikali mbele ya wananchi.

Ameongeza kuwa mafanikio ya NEMC katika utekelezaji wa miradi ya kimazingira pamoja na usimamizi wa Sheria na Kanuni za Mazingira ni ushahidi kwamba viongozi na watumishi wake wameweka maslahi ya Taifa mbele kuliko maslahi binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Sware Semesi amemshukuru Kamishna kwa Tathmini hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ubunifu zaidi kwani pongezi hizo ni chachu ya kuongeza ari ya watumishi kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika ziara yake Kamishna Dk Ndumbaro ameambatana na wataalamu wengine akiwemo Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button