MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Immaculate Semesi ameshiriki kikao cha pili cha majadiliano cha Jukwaa la Wakala wa Utunzaji wa Mazingira Kanda ya Afrika kinachofanyika kuanzia Desemba 3 hadi 5, 2024 Cairo nchini Misri.
Kikao hicho ni kufuatia uzinduzi wa Jukwaa la Wakala wa Utunzaji wa Mazingira Kanda ya Afrika uliofanyika mwaka 2023 mjini Kigali nchini Rwanda ambapo umoja wa Kikanda ulianzishwa chini ya mwamvuli wa ‘Mkutano wa Uwakili wa Mazingira Afrika’ (AMCE).
Kikao hicho kinaratibiwa na Ofisi ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) Kwa kushirikishana na Programu ya Afrika endelevu (ASP) ya kituo cha Mazingira na Maendeleo Cha Kanda ya Uarabuni na Ulaya.
Lengo kuu la kikao hicho ni kufanya mapitio ya malengo ya Jukwaa la Wakala wa Utunzaji wa Mazingira Kanda ya Afrika (AFEPA), mpango mkakati wa utekelezaji, kuunganisha nguvu ili kuchochea vipaumbele vya Kikanda, kushirikishana sera ya utekelezaji na kujadili makubaliano yaliyofanywa na kuchukua hatua zaidi.