UDOM yandaa miradi 11 utekelezaji Dira 2050

DODOMA: CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimesema kimeandaa miradi 11 ya kimkakati ambayo imefikia hatua ya upembuzi yakinifu ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mtaalamu wa masuala ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) wa chuo hicho, Anastazia Njiku, alisema miradi hiyo imeandaliwa na wataalamu wa ndani wa UDOM na inalenga sekta mbalimbali ikiwemo utalii, biashara na huduma, nishati, afya, teknolojia pamoja na michezo.

Akizungumza wakati wa Muhadhara wa Umma uliofanyika chuoni hapo, Njiku amesema maandalizi ya miradi hiyo yanaonesha namna taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kushiriki moja kwa moja katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya nchi.

Amesema miongoni mwa miradi iliyopangwa ni ujenzi wa hoteli ya nyota tano pamoja na uwanja wa mchezo wa golf, mradi wa sanaa na ubunifu, pamoja na kituo cha mikutano cha kimataifa ambavyo tayari vina maandiko ya awali ya upembuzi yakinifu.

“Katika eneo la utalii, tumetenga hekari 125 kwa ajili ya hoteli ya nyota tano na uwanja wa golf. Kwa mradi wa sanaa na ubunifu tumetenga hekari 37, huku kituo cha mikutano cha kimataifa kikitengewa hekari 17,” amesema.

Amefafanua kuwa katika sekta ya biashara na huduma, UDOM imetenga hekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa maduka makubwa ya kisasa (shopping mall), mradi unaotarajiwa kuongeza shughuli za biashara na huduma ndani na nje ya chuo.

Kwa upande wa nishati, amesema chuo kimetenga hekari 400 kwa ajili ya mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia nishati ya jua, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati safi na kuchangia jitihada za taifa za matumizi ya nishati mbadala.

Njiku amesema pia kuna eneo la hekari 2.3 lililotengwa kwa ajili ya mradi wa kituo cha mafuta na gesi asilia, ambalo linatarajiwa kusaidia kuvutia uwekezaji na kuongeza mapato ya chuo pamoja na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya UDOM kuwa kitovu cha ubunifu, uwekezaji na maendeleo, sambamba na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Njiku, utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kufungua fursa mpya za ajira, kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo chuoni na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi utaendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa miradi hiyo, huku chuo kikijipanga kuhakikisha mazingira rafiki yanawekwa kwa ajili ya uwekezaji wenye tija.

Muhadhara huo wa umma umejadili nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kuharakisha maendeleo ya miundombinu na utoaji wa huduma za jamii, sambamba na mchango wake katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button