Kampeni msaada kisheria yarejesha matumaini Pwani
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani, Dk Alice Kaijage amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) imeleta matumaini kwa wananchi wanyonge kutatua migogoro ya ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo mkoani Pwani, Dk Kaijage ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria amesema huduma hizo zinapatikana bure, hivyo wananchi wanapaswa kuzichangamkia.
Amesema, Rais Samia Suluhu Hassan anatosha kwani ameona jinsi wananchi wake wanavyoteseka kwa kukosa huduma za kisheria kwa kuwa hawana uwezo wa kufikia vyombo vya sheria kupeleka changamoto zao.
“Kwa maono yake aliona aje na kampeni ya msaada wa kisheria ambayo haikuwapo kabla, kampeni imefanyika zaidi ya mikoa 15 na matunda yake ni makubwa, hivyo shime wana Pwani muwaambie wenzenu wajitokeze kupata msaada wa kisheria kwenye changamoto zinazowakabili,’’ alieleza.
Pia, alisema kampeni hiyo imekuwa kama shule kwani imechangia upatikanaji wa elimu katika masuala mazima ya sheria na haki zao.
“Hili ni jiwe moja lakini linapiga ndege wengi, wananchi wanapata msaada na elimu kutokana na uamuzi huu wa Rais, amefanya kila linalowezekana kuhakikisha wananchi wanafikiwa kwenye ngazi zote,’’ alisisitiza.



