Kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani na ufanisi wake

MTWARA: KAMPENI ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani ni moja ya mikakati ambayo imesaidia kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Mtwara Mhandisi Hamisi Masindike amesema hayo wakati akiongea na Mwaandishi wa habari hii ofisini kwake.

“Kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ni moja ya mikakati ambayo imesaidia sana kuongeza upatikanaji wa huduma za maji safi na salama Wilaya ya Mtwara hasa vijijini,” amesema.

Amesema kwa sasa upatikanaji wa maji safi na salama Wilaya ya Mtwara umefikia asilimia 58.

“Upatikanaji wa maji umepanda, wakati RUWASA inaanzishwa 2019 upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 50 lakini kwa sasa tumefikia asilimia 58,” amesema.

Amesema RUWASA Wilaya Mtwara vijijni ina jumla ya vijiji 197 na kati ya hivyo ni vijiji 52 tu ndivyo havina huduma ya maji safi kufikia sasa.

“Serikali imeweka mipango kuhakikisha vijiji ambavyo havina huduma ya maji ya RUWASA vinapata maji kabla ya kufikia mwaka 2025,” amesema.

Ameongeza mradi wa Makonde wenye thamani ya Shilingi bilioni 84 ambao unatekelezwa mkoani Mtwara utatoa huduma ya maji kwa vijiji ambavyo havina maji kwa Wilaya za Newala, Tandahimba, Nanyamba mji ikiwemo vijiji vya Mtwara vijijini.

Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 inaelekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji umefikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo 2025.

Habari Zifananazo

Back to top button