Kanuni za usalama zavunjwa Air India

INDIA : MAMLAKA ya Udhibiti wa Safari za Anga nchini India imebaini ukiukaji wa kanuni za usalama 51 katika shirika la ndege la Air India kufuatia ukaguzi wa kila mwaka wa usalama wa anga uliofanyika mwaka jana.
Ripoti hiyo imekuja wiki chache baada ya ajali ya ndege ya Air India aina ya Boeing 787 iliyoua watu 260, ingawa mamlaka imesisitiza kuwa matokeo ya ukaguzi huo hayahusiani moja kwa moja na tukio hilo. SOMA: Air India yapata ajali, yaua
Kwa mujibu wa wakaguzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (DGCA), masuala saba kati ya yaliyobainishwa yalikuwa ya uzito mkubwa, lakini hawakutoa maelezo zaidi kuhusu aina ya changamoto zilizohusika.
Shirika la Air India limesema lilishiriki kikamilifu na kwa uwazi katika ukaguzi huo wa kawaida uliofanyika Julai mwaka jana, ambao unalenga kuboresha utendaji wa mashirika ya ndege nchini humo.
Msemaji wa shirika hilo alisema ni jambo la kawaida kwa mashirika yote ya ndege kufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha viwango vya juu vya usalama na ufanisi katika huduma za anga.
Air India, ambayo ni mojawapo ya mashirika makubwa ya ndege barani Asia, imekuwa chini ya uangalizi mkali wa wadhibiti kufuatia ajali hiyo iliyogharimu maisha ya mamia ya watu na kuzua hofu kuhusu usalama wa anga nchini humo.