Kapinga: Jetour itachochea ajira, ukuaji uchumi

DAR ES SALAAM:Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema ujio wa magari ya Jetour utafungua ukurasa mpya wa fursa za kiuchumi, hasa kuzalisha nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania kwenye nyanja za mauzo, huduma za kiufundi, na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kapinga amesema mbali na kukuza soko la bidhaa, ushirikiano huo ni faida kubwa ya uhamishaji wa teknolojia na maarifa mapya ya kitaalamu nchini kupitia mifumo ya kisasa ya huduma na matengenezo ya magari, mafundi na wataalamu wazawa watapata mafunzo yatakayoinua ujuzi wao, hatua ambayo itaongeza ushindani wa sekta ya magari ya Tanzania na kuinua ubora wa huduma kimataifa.

Vilevile ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kuchochea ukuaji wa mzunguko wa fedha kwenye sekta za usafirishaji, matangazo, na huduma za kifedha, jambo linalodhihirisha jinsi sekta binafsi inavyobaki kuwa injini kuu ya ustawi wa wananchi na maendeleo ya taifa.

Uzinduzi huo, unaotokana na ushirikiano wa kimkakati kati ya Jetour Global na Africarriers Group, unatajwa kuwa hatua kubwa katika kuimarisha sekta ya biashara, kuongeza chaguo kwa watumiaji, na kusukuma mbele ajenda ya serikali ya kukuza uchumi wa kisasa unaoongozwa na sekta binafsi.

Waziri Kapinga amebainisha kuwa uzinduzi huo ni ishara ya mazingira wezeshi ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia maboresho ya sera na sheria za kibiashara. Vilevile, uwekezaji huo unatajwa kuwa mhimili muhimu unaounga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika ujenzi wa uchumi.

Hata hivyo Waziri Kapinga ameipongeza kampuni hiyo kwa  kuichagua Tanzania kuwa kitovu cha kimkakati cha kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha ujenzi wa uchumi jumuishi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button