Karata muhimu Stars leo

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo inashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwakabili Niger katika mchezo wa Kundi F kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Ivory Coast mwezi Januari mwakani.

Stars itahitaji ushindi kuweka matumaini hai kufuzu kwa mara ya tatu kwa fainali hizo kwani mpaka sasa ina pointi ikifungana kila kitu na Uganda ambao watakuwa nyumbani kuwakabili Algeria.

Algeria ilishafuzu fainali hizo baada ya kukusanya pointi 12 ikiziacha kwa mbali Tanzania, Uganda na Niger wanaowania nafasi moja iliyobaki huku Niger ikishika mkia ikiwa na pointi mbili.

Kwenye mchezo wa awali Stars ilitoka sare ya bao 1-1 na Niger kabla ya kufungwa mabao 3-0 na Algeria kisha kuwafunga Uganda bao 1-0 Cairo, Misri na kuja kupoteza kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Uganda.

“Tuna mchezo mgumu unaohitaji matokeo, tunawaheshimu Niger ni timu nzuri lakini naamini kwamba tuko vizuri, tumeyafanyia kazi mapungufu yetu yaliyoonekana katika mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda, tunarudi na mbinu nyingine,” alisema kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemedi Morocco akizungumzia mchezo huo wa leo.

“Sisi kama wachezaji tumejipanga kupambana kupata matokeo na wote tuko tayari kwa ajili ya hilo,” alisema.

Jumla ya wachezaji 30 waliweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo huo muhimu unaohitaji matokeo ya kuamua hatima ya kushiriki fainali za Afrika ‘Afcon’ zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast.

Baada ya mchezo huo dhidi ya Niger, Stars itabakiza mchezo mmoja dhidi ya Algeria utakaochezwa ugenini kumaliza mzunguko wa hatua ya makundi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x