Katambi aahidi kutimiza ndoto za mwanafunzi

DAR ES SALAAM: Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amejitolea kutimiza ndoto ya mwanafunzi Magdalena William Buja (23) mwenye ulemavu wa kutoona kwa kumsomesha na kugharamikia matibabu yake ili kutimiza ndoto yake ya kuwa mwalimu.
Mwanafunzi huyo mwenye ulemavu huo anasoma katika Chuo cha Ufundi na Marekebisho ya Watu wenye Ulemavu Yombo, Dar es Salaam. Alipata ulemavu huo akiwa kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo.
Hayo yamejiri mkoani Dar es salaam wakati Katambi alipotembelea chuoni hapo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya chuo hicho ambapo amesema atahakikisha mwanafunzi huyo anafanyiwa vipimo ili kubaini chanzo cha ulemavu wake.
Amesema majibu ya vipimo yatabainisha kama anaweza kurudi katika hali yake ya awali ama kuendelea na hali hiyo ambapo madaktari watashauri fani anayoweza kusoma ili amsomeshe kuanzia sekondari hadi chuo kikuu.
Akitoa neno la shukrani mwanafunzi huyo, amemshukuru Katambi kwa ujio na uongozi wa chuo kwa kumfundisha kushona nguo licha ya ulemavu alio nao.
3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *