Katavi wanufaika huduma za afya za kibingwa bure

KATAVI; Wananchi wa Mkoa wa Katavi wamepongeza hatua ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Empower Society Build the Nation (ESBN) kuweka kambi maalumu ya huduma za afya bure, wakisema imewasaidia kupata matibabu ya kibingwa ambayo wengi wao walikuwa wakishindwa kuyamudu kutokana na gharama zake.

Huduma hizo zinazotolewa kwa siku saba zinahusisha upimaji wa magonjwa mbalimbali, ushauri wa afya, uchangiaji damu, upimaji wa virusi vya UKIMWI, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, pamoja na matibabu ya macho.

Akizungumza kuhusu huduma hiyo, daktari kiongozi wa timu ya madaktari bingwa wa ESBN, Dk Seif Nassor, amesema lengo la kupeleka tukio hilo Katavi ni kusaidia wananchi kupata huduma za afya karibu na maeneo yao, hasa kutokana na uwepo wa baadhi ya magonjwa ya milipuko kwa maeneo husika.

Amesema mbali na kutoa matibabu, timu hiyo pia inatoa elimu ya afya kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kutambua dalili za magonjwa mapema.

“Wagonjwa wengi wamekuwa wakisumbuliwa na matatizo ya macho bila wao wenyewe kujua, lakini wanapopimwa hugundulika kuwa wana changamoto hizo,” amesema Dk Nassor.

Ameeleza kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa tangu kuanza kwa kambi hiyo, ingawa waliojitokeza kwa wingi ni wazee kuliko vijana.

“Tunaendelea kuhamasisha vijana wajitokeze kwa wingi ili wapate huduma hizi za vipimo na matibabu bure,” amesema.

Amesema ESBN imejipanga kuhakikisha wagonjwa wote wanaopatiwa huduma wanapata mwendelezo wa matibabu hata baada ya kambi hiyo kumalizika, kwa kushirikiana na vituo vya afya na hospitali husika.

“Kwa wagonjwa watakaohitaji upasuaji, tutashirikiana na hospitali ya wilaya kuwafanyia upasuaji kwa sababu tupo na madaktari bingwa wa vitengo mbalimbali,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa ESBN, Goodluck Joseph, amesema kambi hiyo ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo wa kuwafikia wananchi wa maeneo ya pembezoni ambayo mara nyingi hupata huduma za kibingwa kwa ugumu zaidi.

Amesema baada ya Katavi, huduma kama hizo zinatarajiwa kutolewa katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Lindi na Mtwara.

“Tumeelekezwa na Wizara ya Afya kufanya huduma hizi katika mikoa hiyo kutokana na jiografia yake kuwa pembezoni ikilinganishwa na mikoa mingine kama Dar es Salaam, Arusha na Mwanza ambako huduma za kibingwa hupatikana kwa urahisi zaidi,” amesema Joseph.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria kambi hiyo wameiomba ESBN na wadau wengine wa afya kuendelea kupeleka huduma kama hizo katika maeneo yao ili kuwasaidia kupata matibabu ya kibingwa kwa urahisi na kwa gharama nafuu, huku wakieleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema imewapunguzia gharama za matibabu ambazo wengi wao walikuwa hawawezi kuzimudu.

Flora Pesambili, mkazi wa Mpanda, amesema anashukuru kupata huduma hizo kwani zimemsaidia kuokoa fedha ambazo angezitumia kutafuta matibabu hospitalini.

“Tumepokelewa vizuri na tumepunguza gharama ambazo sikuwa na uwezo wa kuzimudu endapo ningekwenda kuzifuata hospitalini,” amesema Pesambili.

Naye Januari Maliganya, mkazi wa Kata ya Misunkumilo, amesema huduma alizopata katika kambi hiyo zingemgharimu kiasi kikubwa cha fedha kama angezipata hospitalini.

“Huduma niliyoipata hapa kama ningekwenda hospitalini ingeweza kunigharimu hadi Sh 150,000, lakini hapa nimetibiwa bure, nashukuru sana na ninaomba zoezi hili liwe endelevu ili wananchi wengi zaidi wanufaike,” amesema Maliganya.

 

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. ★彡[𝐍𝐄𝐄𝐃 𝐏𝐄𝐎𝐏𝐋𝐄 𝐅𝐎𝐑 𝐏𝐀𝐑𝐓 𝐓𝐈𝐌𝐄 𝐎𝐍𝐋𝐈𝐍𝐄 𝐖𝐎𝐑𝐊]彡★

    I get paid over $220 per hour working from home with 2 kids at home. I never thought I would be able to do it but my best friend earns over $35,000 a month doing this and she convinced me to try. it was all true and has totally changed my life… This is what I do, check it out by visiting Following Link…
    .
    You can check more……………… https://Www.Payathome9.Com

  2. I get paid more than $120 to $130 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this i have earned easily $15k from this without having online working skills.
    This is what I do…..    https://www.work27.info

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button