Kaya 16,275 kunufaika majiko ya gesi ya ruzuku Mtwara

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya 50% kwa wananchi wa maeneo ya vijijini mkoani humo.

Sawala ametoa shukrani hizo Januari 2, mwaka huu ofisini kwake mkoani Mtwara wakati wa utambulisho wa mradi na mtoa huduma atakayesambaza majiko hayo mkoani humo ambaye ni Kampuni ya Taifa Gas uliofanywa na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha.Emanuel Yesaya.

“Tumepokea mradi huu ambao unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya na pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi,” alisema Kanali Sawala.

“Mhe. Rais anawapenda wananchi wake, ametuletea mradi nasi tuupokee na tumuunge mkono kwa kununua majiko haya ya ruzuku ili kulinda afya zetu sambamba na kuimarisha mazingira kama alivyoazimia,”alisisitiza Kanali Sawala.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Yesaya alisema REA inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia 2024-2034 kupitia programu mbalimbali ili kufanikisha azma ya Serikali ambayo muasisi wake ni Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na lengo la kulinda afya za wananchi wake pamoja na kuhifadhi mazingira kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tunaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao unaelekeza ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi kupikia,” alifafanua Yesaya.

Aidha, Yesaya alisema kuwa jumla ya majiko ya gesi 16,275 ya kilo sita pamoja na vifaa vyake yatasambazwa katika wilaya tano za Mkoa wa Mtwara ambazo ni Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Newala na Tandahimba ambapo kila wilaya itapata majiko 3,255 na mwananchi atalipia Sh 19,500 tu na kwamba gharama nyingine imebebwa na Serikali.

“Majiko haya yatauzwa kwa wananchi wenye vitambulisho vya NIDA au namba inayoweza kuhakikiwa na hakuna mwananchi atakayeruhusiwa kununua mtungi wa ruzuku zaidi ya mmoja,”alisisitiza Yesaya.

Kwa nyakati tofauti wananchi Mkoani humo wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi huo huku wakihaidi kuendelea kumuunga mkono kwa kuendelea kuhamasishana na kuelimishana ili kufikia azma hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button