Kaya zaidi ya 40 zaagizwa kuhama Same

KILIMANJARO: ZAIDI ya kaya 40 katika Kijiji cha Marieni, Kata ya Chome, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, zimeagizwa kuhama makazi yao kutokana na kusogea kwa ardhi na kutokea kwa nyufa kubwa ambazo tayari zimesababisha uharibifu wa nyumba takribani 10 pamoja na kanisa moja.

Serikali imesema hatua hiyo ni ya haraka kutokana na hatari ya kutokea kwa maporomoko ya ardhi na kuporomoka kwa miamba katika eneo hilo lenye milima na miteremko.

Agizo hilo limetolewa baada ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), chini ya Wizara ya Madini, kufanya utafiti na kubaini mabadiliko ya kijiolojia yanayoendelea chini ya ardhi.

Mabadiliko hayo yameongeza hatari kwa usalama wa wananchi wanaoishi katika eneo hilo, hivyo hatua ya kuwahamisha inalenga kuwalinda dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.

Utafiti huo wa GST umefanyika baada ya kuonekana kwa nyufa kubwa katika eneo hilo, hali ambayo tayari imeanza kusababisha uharibifu wa baadhi ya miundombinu na makazi ya wananchi.

Serikali inatarajiwa kuendelea kufuatilia hali ya eneo hilo na kuchukua hatua stahiki kulingana na matokeo ya utafiti wa kitaalamu, huku wananchi wakitakiwa kuzingatia agizo la kuhama kwa ajili ya usalama wao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button