KENYA : Sheria ya kujitoa uhai yaombwa kufutwa

KENYA : MAHAKAMA Kuu ya Kenya imeamua kuwa kifungu cha 226 cha Kanuni ya Adhabu kinachoharamisha kujitoa uhai kinakiuka katiba ya nchi.
Jaji Lawrence Mugambi amesema sheria hiyo inavunja haki za binadamu, hasa kwa watu wenye matatizo ya afya ya kiakili, kwa kuwahukumu kwa uhalifu badala ya kuwapa matibabu.
Alisema kuwa kifungu hicho kinawalazimisha wahanga wa msongo wa mawazo kuonekana mbele ya jamii kwa aibu, wakati vitendo vyao vinasababishwa na hali ya kiakili.
Aliongeza kuwa sheria hiyo inapingana na haki za katiba za usawa, heshima, na afya. SOMA: Zimbambwe yafuta adhabu ya kifo
Uamuzi huo ulifuata ombi la Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNHCR), Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili (KPA), na Charity Muturi, waliolalamikia kifungu hicho kilichoweka adhabu ya hadi miaka miwili jela kwa kujaribu kujitoa uhai.
Serikali kupitia Wizara ya Afya inatambua kujiua kama tatizo la afya ya umma na ina mkakati wa kupambana nalo hadi mwaka 2026.



